Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MHADHIRI UDOM KIZIMBANI KWA RUSHWA YA NGONO

Na Faustine Gimu Galafoni,Dodoma.
Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa nchini  [TAKUKURU ]mkoa wa Dodoma  inatarajiwa kuwafikisha mahakamani watu 10 katika mahakama za Dodoma na Bahi na kuwafungulia mashauri yanayohusiana na Rushwa akiwemo Mhadhiri Msaidizi Chuo kikuu cha Dodoma akihusihwa na rushwa ya ngono.


Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Agosti 13,2020 jijini Dodoma,Mkuu wa TAKUKURU mkoani hapa Bw.Sosthenes Kibwengo amesema kwa kushirikiana na ofisi ya taifa ya mashtaka ,TAKUKURU mkoani Dodoma itamfikisha mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma Bw.Jacob Paul Nyangusi [43]mhadhiri Msaidizi wa chuo kikuu cha Dodoma[UDOM]na kumfungulia shauri la uhujumu uchumi kwa kosa la kutaka rushwa ya ngono kinyume na kifungu cha 25 cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa Na.11 /2007 ikisomwa pamoja na aya ya 21 jedwali la kwanza na vifungu vya 57[1]na 60[2] vya sheria ya uhujumu uchumi   sura ya 200 marejeo ya mwaka 2020.

Bw.Kibwengo amefafanua kuwa,Majira ya saa 3 usiku   wa tarehe 3,Oktoba,2018 TAKUKURU ilimkamata Bw.Nyangusi nyumbani kwake  eneo la  Nyumba Mia tatu jijini Dodoma muda mfupi kabla hajatekeleza nia yake ovu ya kufanya ngono  na aliyekuwa mwanafunzi wake wa mwaka wa kwanza wa shahada ya sanaa katika jiografia na Mazingira.

Mkuu huyo wa TAKUKURU mkoani Dodoma,ameendelea kufafanua kuwa ,awali TAKUKURU ilipokea taarifa kuwa mtuhumiwa alimtaka  mwanafunzi wake  huyo kingono kama sharti la kumsaidia ili aweze kufanya mitihani ya marudio na kumwezesha kufaulu katika somo lake ,na ndipo ikaweka mtego na kumkamata.

Aidha,Bw.Kibwengo amesema TAKUKURU Dodoma kwa kushirikiana na ofisi ya Taifa ya Mashtaka watafikishwa mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma watu watatu ambao ni Diwani Mstaafu kata ya Ntyuka jijini hapa Bw.Theobald Emmanuel Maina [44],Afisa Mtendaji Mstaafu kata ya Ntyuka Bw.Benedict Baraguyu Mazengo[60] na Mwenyekiti mstaafu mtaa wa Chimala jijini Dodoma Bw.Anderson Jonathan  Mwaluko[48] kwa makosa ya matumizi mabaya ya mamlaka kinyume na kifungu cha 31 na ubadhirifu kinyume na kifungu cha 28[1]vyote vya sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa  Na.11/2007.

“Uchunguzi wetu  umeonesha kuwa ,April,2016 watuhumiwa kwa pamoja walitumia vibaya madaraka yao na hivyo kujipatia n kwa njia ya kughushi Tsh.Milioni mbili ambazo ni malipo ya minara ya simu iliyopo kwenye kata ya Ntyuka ,watuhumiwa walifuja frdha hizo badala ya kusimamia ili zitumike kwa ajili ya kununua vifaa vya ujenzi wa ofisi ya Mtaa wa Ntyuka”amesema Bw.Kibwengo.

Bw.Kibwengo amesema TAKUKURU,Dodoma itamfikisha mahakamani  afisa mtendaji Mstaafu kata ya Mnadani Bi.Ritha Protas [30] kwa kosa la kuomba rushwa Tsh.Laki nne kinyume na kifungu cha 15[1]cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa  Na.11/2007.

“Uchunguzi wetu umeonesha kuwa  Tarehe 17,Mei,2019 mtuhumiwa aliwashawishi wanakikundi cha Sabasaba Group ambao walikuwa wanafuatilia mikopo inayotolewa na halmashauri ya jiji  kwa ajili ya wajasiriamali  wampatie fedha hizo ili awasaidie kupata mikopo na baada ya wanakikundi hao kukosa mikopo kama walivyoahidiwa na mtuhumiwa waliamua kwenda  Ofisi za Halmashauri za jiji kutoa taarifa na walipotambua kuwa huo sio utaratibu wa  kupata mikopo,walitoa taarifa TAKUKURU na ndipo uchunguzi ukafanyika na kuthibitika alipokea kiasi hicho alichoshawishi”amesema.

Bw.Kibwengo pia amesema TAKUKURU itamfikisha mahakama ya Wilaya ya Bahi mtendaji wa  kijiji cha Chifutuka Bw.Alfred Ndukai Oleteya[58] na kumfungulia shauri la jinai la kuomba na kupokea rushwa ya Tsh.Laki mbili kinyume na kifungu cha 15[1]a cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa  Na.11/2007.

Hali kadhalika,TAKUKURU mkoani Dodoma inatarajia kuwafikisha katika mahakama ya wilaya ya Bahi watu wanne  ambao ni Afisa Misitu wa Bahi Bw.Said Msemo[56],Ramadhan Juma Said[35]Msaidizi wa  afisa misitu ,Bw.Michael Robert[34],na Bw.Molo Lucas Mwalise [40]Mgambo wa kijiji cha Lamaiti-Bahi kwa makosa ya kuomba rushwa ya Tsh.Laki tano na kupokea laki moja na elfu hamsini kutoka kwa mwananchi mmoja ili wamrejeshee pikipiki yake waliyoikamata awali.

Vilevile Bw.Kibwengo amesema Mahakama ya Kondoa imetoa uamuzi wa shauri la uhujumu uchumi  Na.3/2018  na kumtia hatiani hukumu ya Mwaka mmoja jela au faini ya Tsh.       Mil. Moja  pamoja na  kurejesha Tsh. Mil.7 .25 Bi.Bunana Dioniz Msafiri  afisa mifugo mstaafu halmashauri ya mji wa Kondoa  ambapo Agosti 2018 TAKUKURU ilimfikisha Mahakamani kwa matumizi mabaya ya mamlaka   aliyosababisha hasara  ya  Tsh.Mil.7.25 za ushuru wa machinjio  alizokusanya bila kuwasilisha halmashauri.

Sanjari na hayo,TAKUKURU mkoani Dodoma  Mwezi Julai 2020 imefanikiwa kuokoa  mbao 106 zilizokuwa zimevunwa na kuhifadhiwa kinyume na taratibu  katika nyumba ya mwananchi mmoja kijiji cha Lamaiti Wilayani Bahi .

MWISHO.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com