NA MWAMVUA MWINYI,PWANI
JESHI la polisi mkoani Pwani, linamshikilia mwalimu Evata Mboya,wa shule ya msingi Mwendapole,Kibaha, kwa kosa linalodaiwa ni kumshambulia kwa fimbo mwanafunzi na kumsababishia maumivu makali ya kichwa.
Mwanafunzi huyo wa darasa la tano ,miaka 12 ,walipewa adhabu ya kuchapwa fimbo na wenzake ambao walikuwa wakipiga kelele darasani.
Kamanda wa polisi mkoani Pwani, Wankyo Nyigesa alithibitisha kuhusu tukio hilo na kusema ,mwalimu huyo alitoa adhabu kwa wanafunzi 15 waliokuwa wanapiga makelele darasani ambapo walipigwa fimbo tatu kila mmoja.
Alieleza,baada ya muda walimu wakiwa ofisini walishangaa kuona wanafunzi wengine wakiwa wamembeba mtoto huyo huku akilalamika maumivu makali ya kichwa ,hali iliyosababisha kumpeleka hospital ya Tumbi na hali ilizidi kuwa mbaya ambapo mtoto huyo alihamishiwa hospital ya Mloganzila kwa matibabu zaidi .
Wankyo alifafanua ,mtoto anaendelea na matibabu na mwalimu Evata anaendelea kushikiliwa na polisi huku upelelezi ukiendelea kufanyika na baada ya upelelezi kukamilika atafikishwa mahakamani.
Wakati huo huo,jeshi la polisi likiwa doria eneo la Ruvu JKT ,Mlandizi,lilifanikiwa kumkamata dereva Alfajiri Kibonda (33)wa USA River ,Arusha akiwa na gari yenye namba za usajili T.173 CMK aina ya Toyota Chaser,ambayo inadhaniwa ni gari la wizi .
Wankyo alibainisha,dereva huyo hana nyaraka halali hivyo amewataka wananchi kama yupo aliyeibiwa gari tajwa na akiwa na nyaraka halali afike katika jeshi hilo .
Katika hatua nyingine Shaban Salum (70)mkazi wa Mkange ,Chalinze na Ally Hussein (79) mkazi wa Bwilingu wamekamatwa na polisi kwa kosa la kumiliki silaha aina ya gobore ambazo hazina vibali vya umiliki .
Wankyo aliiasa jamii kutoa ushirikiano wa taarifa ya wahalifu wowote , kwa jeshi hilo ili kupambana na uhalifu mkoani humo .
Social Plugin