Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

NDEGE YA SHIRIKA LA NDEGE TANZANIA (ATCL) AINA YA BOMBARDIER Q400 KUTUA SONGEA SEPTEMBA MWAKA HUU


Ndege ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) aina ya Bombardier Q400, inatarajia kuanza safari za kuruka na kutua katika Kiwanja cha Ndege cha Songea kuanzia mwezi ujao ili kufungua fursa za kiuchumi na kijamii.


Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, alisema hayo jana mjini hapa akiwa mkoani Ruvuma kwa ziara ya kikazi ya siku mbili kukagua hali ya miundombinu ya barabara, madaraja na kiwanja cha ndege.

Kamwelwe alisema ameridhishwa na hatua zilizofikiwa za ukarabati wa kiwanja hicho ikiwamo uboreshaji wa barabara ya kutua na kuruka yenye urefu wa mita 1,740, maegesho na taa za kuongozea ndege.

“Hadi sasa hatua zilizofikiwa ni nzuri na kufikia mwisho wa mwezi huu, mkandarasi atakuwa amekamilisha kujenga mita 1,200 za barabara ya kuruka na kutua ndege ambayo itaruhusu ndege kubwa aina ya Bombardier kuanza kutua,” alisema.

Waziri Kamwelwe alisema ukarabati na uboreshaji wa kiwanja hicho unagharimu Sh. bilioni 37 ambazo ni fedha za ndani na unatarajiwa kukamilika Desemba, mwaka huu.

Pia aliongeza kuwa kukamilika kwa kiwanja hicho kutarahisisha usafirishaji wa abiria na mizigo katika ukanda wa kusini ambao awali ulikuwa na changamoto kubwa ya usafiri wa anga.

“Ujio wa ndege hizi utapunguza gharama za usafiri wa ndege. Awali gharama ya ndege ilikuwa fedha za kitanzania Sh. 500,000 tano kwa safari moja na hii ilisababisha watu wachache kumudu gharama hizo,” alisisitiza.

Waziri Kamwelwe alisema azma ya serikali ni kuendelea na uboreshaji na ukarabati wa viwanja vingine 10 nchini kwa lengo la kuinua na kukuza uchumi wa taifa.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com