Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) nchini Tanzania, imesema idadi ya wapiga kura katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Jumatano Oktoba 28 2020 ni milioni 29 huku vituo vya kupiga kura vitakuwa 80,155.
Idadi hiyo imetajwa leo Jumamosi tarehe 1 Agosti 2020 na Jaji Semistocle Kaijage, Mwenyekiti wa NEC katika kikao cha tume hiyo na viongozi wa vyama vya siasa kuhusu maandalizi ya uchaguzi huo.
Jaji Kaijage amesema, baada ya mazoezi mawili ya uboreshaji wa daftari la wapiga kura kukamilika, daftari hilo lina wapiga kura 29,188,347.
Akizungumzia mkutano huo, Jaji Kaijage amesema, NEC imewaita wadau wa uchaguzi ili kubadilishana nao mawazo juu ya namna ya utekelezaji wa shughuli za uchaguzi huo, ili kuepusha dosari zinazoweza kuathiri uchaguzi.
Amevitaka vyama vya siasa kuchagua watu makini ili kuepusha migogoro baina yao na Tume, pindi wanapotakiwa kukamilisha mchakato wa kupitisha majina ya wagombea.
Amesema kuwa fomu za uteuzi zitaanza kutolewa Agosti 5, 2020, kwenye makao makuu ya ofisi za Tume jijini Dodoma kwa wagombea wa kiti cha Urais huku Wabunge na Madiwani watafuata fomu hizo katika makao makuu ya Halmashauri ya Majimbo na Kata husika.
“Fomu zitaanza kurejeshwa muda wowote pindi mgombea anapomaliza kujaza kwa usahihi hadi Agosti 25 saa 10 jioni, ambayo ndiyo itakuwa siku ya uteuzi, naomba mjaze kwa usahihi bila dosari yoyote ili usijekosa sifa na usiteuliwe na kuanza lawama”, amesema Jaji Kaijage.
Jaji Kaijage ameongeza kuwa, “Wale wote wenye malalamiko na tume tunaomba mtuletee wenyewe tutayafanyia kazi, ila sio kulalamikia mitandaoni hatutajihusisha na malalamiko ya mitandaoni”.