Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Prof. Luoga: Uimara Wa Sekta Ya Fedha Unaongeza Huduma Jumuishi Za Kifedha

Na. Peter Haule na Farida Ramadhani, WFM, Simiyu
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Prof. Florens Luoga, amesema kuwa Wizara ya Fedha na Mipango imejielekeza katika kuikwamua Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa kuweka Sheria ambazo zinahakikisha kuimarika kwa huduma jumuishi za kifedha.

Prof. Luoga, aliyasema hayo alipotembelea Banda la Wizara ya Fedha na Mipango katika Maonesho ya Nanenane yanayofanyika Kitaifa katika Viwanja vya Nyakabindi Mkoani Simiyu.

“Ushiriki wa Idara na Taasisi za Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na Mabenki umeongezeka, hii ni jambo zuri kwa kuwa ni Sekta muhimu katika kukuza sekta ya Kilimo, Uvuvi na ufugaji inayochukua watanzania wengi zaidi ya asilimia 70”, alisema Prof. Luoga.

Aidha alisema kuwa BoT imejiimarisha zaidi kwa kushirikiana na Mabenki, kuhakikisha kuwa huduma za kifedha na uwekezaji katika sekta binafsi inapewa kipaumbele, kila benki iliyokuja katika maonesho ya Nanenane kwa mwaka huu ina bidhaa maalum kwa ajili ya kuhudumia sekta hizo, kitu ambacho ni mwamko mpya unaotokana na Sera bora za Serikali.

Prof Luoga alisema kuwa kuimarika kwa sekta ya fedha kwenye kilimo, mifugo na uvuvi kutaondoa tatizo la uzalishaji wa msimu kwa kuwa viwanda vinavyotegemea malighafi za kilimo vinaweza kusimama muda wowote kama vitakosa malighafi hizo.

Alisema Sera zinahimiza kuhuisha mifumo ya umwagiliaji, mamlaka zinazohifadhi mazao na nafaka hivyo kuhakikisha mazao yanayohitajika kuchakatwa yanapatikana kipindi cha mwaka mzima.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mara, Bw. Adam Malima, amesema kuwa watanzania wanatakiwa kutambua kuwa kodi zinazotozwa  na Serikali zina tija kwa wakulima na zinasaidia kuboresha maisha na uzalishaji.

Alisema kuwa kuna kodi ambazo ni kero kwa wakulima na wavuvi ambazo Serikali kupitia Wizara ya Fedha imeziondoa, jambo ambalo lina manufaa makubwa kwa uchumi wa nchi kwa kuwa linachochea uzalishaji.

“Nimetembelea Banda la Wizara hii mwaka  wa tatu mfululizo na kila nilipofika nimekuta kuna ongezeko la huduma na ubunifu mkubwa jambo linaloashiria kuna dhamira ya dhati ya kukuza uchumi wa nchi kupitia huduma za kifedha hivyo mnastahili kupongezwa”, alieleza Bw. Malima.

Nidhamu inayooneshwa na Wizara ya Fedha na Mipango katika Mapato na Matumizi kupitia mifumo iliyoanzishwa ni vema ikapelekwa katika ngazi zote kwa watendaji wa Serikali hususani wanaoshughulikia masuala ya fedha za umma ili kuongeza mapato na usimamizi wa mapato hayo.

Akiwaongoza wageni hao kutembelea Banda la Wizara ya Fedha na Mipango, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Seikalini wa Wizara hiyo, Bw. Benny Mwaipaja, aliuhakikishia Umma kwamba Serikali inatambua mchango wa Sekta ya kilimo katika kukuza uchumi wa nchi hivyo itaendelea kuandaa Sera nzuri za fedha na bajeti ili kukuza uchumi wa nchi.

Alisema kuwa baada ya kubuniwa kwa Mfumo wa Kielektroniki wa Kukusanya Mapato ya Serikali GePG kwa kutumia wataalamu wake wa ndani, hivi sasa wataalam hao wamebuni mfumo mwingine wa kiuhasibu ujulikanao kwa jina la MUSE, unaolenga kusimamia matumizi ya Serikali ambao umeanza kutumika.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com