Na Jonas Kamaleki
Serikali imezitaka benki na taasisi nyingine za fedha kukopesha miradi mikubwa ya uchimbaji wa madini nchini ili kukuza sekta hiyo ambayo imeanza kutoa mchango mkubwa kwenye pato la taifa.
Akifungua mafunzo haya leo jijini Dodoma, Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo amesema imekuwa ndoto yake ya muda mrefu ya Tume ya Madini kukutana na mabenki kwa ajili ya mustakhabali wa wachimbaji wa madini.
“Sekta ya madini kufungamanishwa na mabenki ni hatua kubwa katika kukuza sekta hiyo ambayo ina mchango mkubwa kiuchumi kwa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla”, amesema Nyongo.
Waziri Nyongo amebainisha ukuaji wa haraka wa sekta ya madini nchini na kusema kuwa miaka michache iliyopita sekta ya madini ilikuwa ikichangia aslimia 3.8 kwenye pato la Taifa lakini kwa sasa inachangia zaidi ya asilimia 5.2, ameongeza kuwa sekta hiyo inakuwa kwa asilimia 17.7.
Amesisitiza elimu ya biashara ya madini kuendelea kutolewa kwa mabenki ili kuwajengea uwezo wakopeshaji ili kutambua fursa zilizopo kwenye sekta ya madini na kuwataka kuajiri wataalaam wa madini ambao wanaweza kuchambua michanganuo ya mikopo ya uchimbaji wa madini.
“Natoa wito kwa mabenki mengine kupitishwa kwenye mafunzo haya ili waweze kuwakopesha wachimbaji hasa wadogo na kwa kufanya hivyo kipato chao kitaongezeka, ajira zitaongezeka na mabenki yatafanya biashara kutokana na riba”, alisema Nyongo.
Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo, Katibu Mtendaji Tume ya Madini, Prof. Shukrani Manya amesema kuwa sekta ya madini ni sekta muhimu katika uchumi ambayo inahitaji mitaji mikubwa katika uwekezaji wake hivyo watoa mikopo ni muhimu kuwa na uelewa wa sheria na kanuni za madini.
“Sekta ya madini ni biashara kama biashara nyingine inahitaji mitaji mikubwa hivyo ninyi watu wa benki inabidi mjue vizuri leseni za madini, uhai wa leseni hizo na sheria na kanuni za madini”, alisema Prof. Manya.
Aidha, Prof. Manya amesema mafunzo hayo yataondoa kusitasita kutoa mikopo kwa wachimbaji hasa wadogo baada ya kuwa na uelewa mpana kuhusu mnyororo wa madini unaohusu wachimbaji, wauuzaji, vifaa vya uchimbaji na uchakataji wa madini na watoa huduma wengine katika sekta hiyo.
Prof. Manya ameyaomba mabenki mengine kujengewa uwezo na kutoa mikopo kwa wachimbaji wa madini kwa kuzingatia vigezo vilivyopo ikiwemo uhai wa leseni ya mchimbaji.
Kwa upande wake Mratibu wa Mafunzo hayo, Meneja wa Dawati Maalum la Wateja wakubwa Fredrick Mwamyalla amesema benki ya CRDB kwa kushirikiana na Tume ya Madini imeandaa mafunzo hayo kutokana na mageuzi yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano ikiwemo kuanzisha masoko ya madini, kurekebisha Sheria ya Madini na kudhibiti mianya ya utoroshaji madini.
“Kupitia mafunzo haya tutakuwa na nafasi nzuri zaidi ya kubuni bidhaa nzuri zinazohusu utoaji mikopo kwa sekta ya madini, hasa kwa wachimbaji wadogo, wakubwa na wa kati”, alisisitiza Mwamyalla.
Mwamyalla ametoa wito kwa wachimbaji, wanunuzi na wauzaji wa madini kufika CRDB Benki ili kupata mikopo ya kuwawezesha kuwekeza katika sekta hiyo.
Maafisa Waandamizi wa Benki ya CRDB wamepewa mafunzo kuhusu sekta ya madini ili kujengewa uwezo katika sekta hiyo ili kurahisiha utoaji mikopo kwa wachimbaji wadogo, wa kati na wakubwa ikiwemo watoa huduma.
Mafunzo hayo ambayo yameanza leo (Agosti 6, 2020) jijini Dodoma yanatolewa na wataalaam toka Tume ya Madini.
Mafunzo hayo yanafanyika kwa siku mbili ambapo mada mbalimbali zitawasilishwa kwa. Baadhi ya mada ni Sheria na Kanuni za Madini, Jiolojia na Madini yanayopatikana nchini na Leseni za Madini. Mafunzo hayo ni mwendelezo wa kuyajengea uwezo mabenki kwani yalianza kutolewa kwa benki ya NMB.
Social Plugin