Mshambuliaji wa Simba, Christopher Mugalu akipongezwa na Clotous Chama baada ya kuifungia timu yake bao la tano.
**
Wekundu wa Msimbazi wamehitimisha kilele cha tamasha la Simba Day na Wiki ya Mabingwa hao 'CHAMPIONS WEEK: Another Level katika SIMBA DAY' kwa kuibuka na ushindi mnono wa mabao 6-0 dhidi ya wageni wao, Vital'O Club ya Burundi.
Mabao ya Simba yamefungwa na Bernard Morrison, John Bocco, Ibrahim Ajibu, Clotous Chama, Christopher Mugalu na Charles Ilanfya.
Imekuwa kawaida kwa mwaka wa 12 sasa, Simba SC kuzindua msimu mpya kwa tamasha kubwa linalopambwa na burudani ya muziki kabla ya kutambulisha kikosi cha msimu kwa mchezo wa kirafiki.
Na leo baada ya burudani zilizoongozwa na msanii nyota zaidi nchini, Nassib Abdul ‘Diamond Platnumz’ ukawadia mchezo huo wa kirafiki, ambao kikosi cha Wekundu wa Msimbazi kiliwapa furaha mashabiki wao.
Hadi mapumziko Simba SC walikuwa mbele kwa 2-0, kazi nzuri ikifanywa na kiungo mpya wa kimataifa wa Zambia, Rally Bwalya akiseti mabao yote hayo.
Morrison alifunga bao la kwanza dakika ya 44 kwa shuti la mguu wa kulia kufuatia pasi ndefu na nzuri ya mchezaji wa zamani wa Power Dynamos ya Zambia, Bwalya.
Morrison naye akapokea pasi nyingine nzuri ya Bwalya na kumtilia krosi nzuri ya chini Nahodha na mshambuliaji John Raphael Bocco aliyefunga bao la pili dakika ya 45 na ushei.
Kipindi cha pili kocha wa Simba SC, Mbelgiji Sven-Ludwig Vandenbroeck alibadili kikosi kizima amacho kilikwenda kutanua ushindi hadi mabao matano.
Kiungo mwingine Mzambia, Clatous Chotta Chama alifungua shangwe za mabao kipindi cha pili kwa kufunga la tatu dakika ya 56 baada ya kumlamba chenga beki wa Vital’O na kufumua shuti kufuata krosi nzuri ya Ibrahim Ajibu Migomba kutoka kulia.
Ajibu mwenyewe akafunga bao la nne dakika ya 76 akimalizia pasi ya Chama, kabla ya mchezaji mwingine mpya, mshambuliaji Mkongo Chriss Mugalu aliyesajiliwa kutoka Lusaka Dynamos kufunga la tano.
Winga mpya, Charles Ilamfya aliyesajiliwa kutoka KMC ya Kinondoni akaitelezea krosi ya chini ya Nahodha Msaidizi, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ kutoka upande wa kushoto kufunga bao la sita dakika ya 90 na ushei.
Bernard Morrison akifurahia baada ya kuifungia timu hiyo bao la kwanza
Nahodha wa Simba, John Bocco baada ya kufunga bao la pili kwa timu yake katika mchezo huo
Picha kwa hisani ya Simba SC Tanzania
Social Plugin