Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TMDA YAFUNGUA MASHAURI 146 KWA WATUHUMIWA MAKOSA YA UKIUKWAJI WA SHERIA

 Meneja wa Huduma za Sheria wa TMDA, Wakili Iskari Fute akizungumza katika kikao kazi cha Uhamasishaji wa Waandishi wa Habari kuhusu Usimamizi wa Sheria ya Dawa na Vifaa Tiba.
Baadhi ya Wanahabari wa Mikoa ya Morogoro, Pwani na Dar es Salaam wakiwa katika picha ya pamoja na maafisa waandamizi wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) wakati wa kikao elekezi mjini Morogoro.


Na Andrew Chale - Morogoro

MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba nchini, (TMDA) imebainisha kuwa, hadi sasa imefungua mashauri 146 kutokana na watu kukiuka sheria za mamlaka hiyo.

Hayo yameelezwa Mjini hapa na Meneja wa Huduma za Sheria, Wakili Iskari Fute, wakati  wa kuwasilisha mada kuhusu Usimamizi wa Sheria ya Dawa na Vifaa Tiba katika kikao kazi cha Uhamasishaji wa Waandishi wa habari   kutoka Mikoa ya Morogoro, Dar es Salaam na Pwani.

Fute alibainisha kuwa, TMDA imekuwa ikifuatilia kwa karibu masuala yote ya kisheria na kuchukua hatua mbalimbali kwa watuhumiwa ikiwa ni kulinda afya ya jamii. 

"Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita hadi kufikia sasa TMDA imefungua mashauri 146. 

Kati ya mashauri hayo 146, yaliyokwisha  na watuhumiwa kuchukuliwa hatua kali ikiwemo kulipa faini ni 32.

Lakini pia mashauri mengine 32 pekee ndio yamebaki hadi sasa na mashauri 82 uchunguzi wake unaendelea katika Mahakama na vituo vya Polisi." Alisema Fute.

Fute alibainisha kuwa, watuhumiwa hao waliofunguliwa mashauri baada ya TMDA kufanya kaguzi mbalimbali za kushtukiza katika maeneo tofauti ikiwa ni lengo la mamlaka kulinda afya ya jamii kupitia sheria ya Dawa na Vifaa Tiba sura ya 219.

Aidha, Alieleza msingi wa sheria ya TMDA ni Katiba ya Jamhuri ya Muungano. Sura ya 2 ibara ya 63 (c) na 64.
Ambapo Ibara hizo zinaweka mamlaka ya Bunge kutunga sheria zote.

"Kwa vile haki ya kuishi kwa kila mtu inalindwa na Katiba, ni wazi kuwa sheria ya TMDA inatekeleza masharti ya Katiba ya haki ya kuishi kwa vile jukumu lake ni KULINDA AFYA ZA WATANZANIA". Alimalizia Fute 

Kwa upande wake, Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Morogoro, Anza Ndossa aliyekuwa Mgeni rasmi, aliwataka Wanahabari kutumia taaluma yao kufikisha elimu pamoja na kufichua wakiukwaji wa sheria za dawa na vifaa tiba.

"Kupitia ninyi na Vyombo vyenu vya Habari wananchi watapata taarifa sahihi ya kujua dawa duni na pia kulinda afya zao" alisema Ndossa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com