WAKULIMA NCHINI WASHAURIWA KUJIKITA KWENYE KILIMO CHA UMWAGILIAJI

Na Innocent Natai, Lindi

Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga awataka Wakulima kuachana na Kilimo cha kutegemea Mvua na badala yake kutumia maji ya Mito na Mabwawa kwa kufanya Kilimo cha umwagiliaji ili kuwasaidia kuondoakana na changamoto ya upungufu wa mvua  kwani ndio njia itakayo wawezesha Kulima Kilimo chenye tija.

Ameyasema hayo wakati akizungumza na wakulima wa zao la Korosho  katika Kijiji cha Tingi, Wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi wakati akiendelea na ziara yake kwa siku ya pili ya kusikiliza na kutatua kero na changamoto zinazowakabili wakulima wa zao la Korosho.

Hasunga amesema suala la Upungufu wa mvua limekuwa likitumiwa na wakulima kama sababu inayopelekea ukosefu wa mazao ya kutosha hivyo ni vyema sasa wakajikita katika matumizi ya maji ya Mito na Mabwawa katika Kilimo kwani mbali na kuondoa changamoto ya upungufu wa maji pia itawawezesha kuondokana na Kilimo cha msimu kisichikuwa na tija hivyo wataweza Kulima kwa kipindi kirefu bila ya kupumzika huku wakinufaika na Kilimo hicho.

Amewataka wakazi wa Kilwa kutumia vizuri Bonde la mto Rufiji kwa ajili ya kufanya shughuli za kilimo kwani ni eneo lenye maji ya kutosha kwa ajili ya umwagiliaji na lenye rutuba ya kutosha kwa ajili ya Kilimo.

“Bonde la mto Rufiji likitumika ipaswavyo lina uwezo wa kuzalisha chakula cha kutosha kwa mwaka mzima lakini kwa sasa halitumiki ipaswavyo ni mapori tu yamejaa” Amesema

Aidha, amesema kuwa serikali kupitia Wizara ya Kilimo imedhamiria kuhakikisha inatumia fursa ya uwepo wa Mradi wa kufua umeme unaotokana na maporomoko ya maji ya Mto Rufiji maarufu kama Stiglers.

Kwa kuwasaidia wakulima na watanzania wanaoishi chini ya mradi huo kunufaika na mradi huo kwa kuwawawekea miundombinu ya umwagiliaji ili waweze kufanya kilimo cha kisasa ambacho kitakuwa ni cha mwaka mzima hivyo kuinua pato la Mkulima na Taifa kwa ujumla.

Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga  anatarajiwa kumaliza ziara yake ya Siku tatu ya kutembelea, kuskiliza na kutatua kero zinazowakabili  Wakulima wa zao la Korosho katika baadhi ya Wilaya za Mikoa ya Pwani na Lindi ambapo leo atahudhuria Mkutano wa Wadau wa Korosho utakaofanyikia Mkoani Lindi.

MWISHO


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post