Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WALIMU WA SHULE ZA MSINGI NA SEKONDARI KATIKA MANISPAA YA ILEMELA WAPATIWA HATI ZA ARDHI

Na Munir Shemweta, WANMM ILEMELA

Naibu waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi  Dkt Angeline Mabula ametoa hati 315 kwa walimu wa shule za Msingi na Sekondari katika Manispaa ya Ilemela ikiwa ni juhudi zake za kuhakikisha walimu wa maniapaa hiyo wanamilikishwa ardhi kwa gharama nafuu.

Walimu waliopatiwa Hati za viwanja ni sehemu ya walimu 525 walioomba kupatiwa viwanja katika eneo la Nyamiswi Manispaa ya Ilemela ambapo wengine walishindwa kukamilisha malipo ya viwanja hivyo.

Akizungumza wakati wa kugawa hati hizo kwa walimu wa shule za msingi na sekondari za Manispaa ya Ilemela Dkt Mabula mbali na kuwapongeza walimu hao kwa kukamilisha malipo hadi kumilikishwa ardhi na kuwataka  kuzitumia hati hizo kwa shughuli za maendeleo.

Aidha, Dkt Mabula ambaye ndiye aliyewahamasisha walimu hao kujiunga pamoja kwa ajili ya kupata viwanja aliyataka makundi mengine maalum kujiunga pamoja kwa lengo la kuona namna ya kuyasaidia kupata viwanja katika halmashauri ya Manispaa ya Ilemela.

"Suala la makazi siyo la walimu pekee tuone kama kuna kundi lingine maalum nalo likajiunga kama walivyojiunga walimu na kuchangia  fedha ili kupatiwa viwanja" alisema Naibu Waziri Mabula.

Kwa mujibu wa Dkt Mabula kilichofanyika kwa walimu wa Manispaa ya Ilemela ni juhudi za Rais John Pombe Magufuli kutaka kila mwenye ardhi awe na umiliki ili kujua mipaka yake na kupata hati kwa lengo la kupunguza migogoro ya ardhi na wakati huo kuitumia hati  kwa shughuli za maendeleo.

Aliwaasa walimu kutumia mabenki ikiwemo benki ya NMB kuomba mikopo ya ujenzi wa nyumba ili kuwezesha eneo walilopata kwenda kwa kasi hasa ikizingatiwa eneo hilo limepakana na eneo la Chuo Kikuu cha Mzumbe, Chuo cha Afya na Hospitali ya Wilaya ya Ilemela na kubainisha kuwa eneo hilo ni zuri na hata kama walimu hao hawatakaa wanaweza kupangisha na kuingiza fedha kidogo kidogo.

Kwa upande wake Katibu wa Kamati ya mradi wa viwanja vya walimu katika halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Albert Mahuyu alisema pamoja na kamati yake kukutana na changamoto kadhaa wakati wa zoezi hilo ikiwemo baadhi ya walimu kushindwa kukamilisha malipo kwa wakati lakini imefanikisha upimaji viwanja 525 na kuingiza kiasi cha shilingi milioni 404.

Naye Meneja wa NMB kanda ya Ziwa Baraka Ladislaus alisema benki yake iko tayari kutoa mikopo kwa walimu na kubainisha mikopo inayotolewa na benki hiyo kuwa ni ile ya kununua, kuezeka na kumalizia nyumba pamoja na mkopo wa kurudishiwa fedha uliyojengea nyumba na mikopo iko hadi ya milioni 200 na unarejesha kidogokidogo kwa takriban miaka mitano.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com