Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAZIRI BASHUNGWA ASEMA MFUMO WA CRDB WAKALA UNACHOCHEA UKUAJI SEKTA YA FEDHA NCHINI


IMG-20200806-WA0025
Waziri wa Viwanda Innocent Bushungwa ameipongeza Benki ya CRDB kwa kuwa mstari wa mbele katika kusaidia jitihada za Serikali katika kuhakikisha Watanzania wengi wanapata fursa ya kujiunga na mfumo rasmi wa kibenki hususani maeneo ya vijijini. Bashungwa alisema hayo wakati wa ufunguzi wa Semina ya CRDB Wakala iliyofanyika Wilayani Bariadi Mkoa wa Simiyu.

Sekta ya fedha ni kichocheo muhimu cha maendeleo ya taifa letu. Lakini ili sekta ya fedha iweze kutoa mchango unaokusudiwa, inapaswa iwe imara, na iwe na uwezo mkubwa wa kufikia wateja wengi mijini na vijijini” alisema Bashungwa.

Akiipongeza Benki ya CRDB kwa kupanua wigo wake wa utoaji huduma kupitia mfumo wa mawakala ujulikanao kama CRDB Wakala, Bashungwa alisema ili kuendana na kasi ya maendeleo nchini Benki zinapaswa kuwekeza katika mifumo ya kidijitali inayotoa fursa ya kubuni njia mbadala za utoaji huduma kwa wateja.

“Nimefurahi kusikia sasa hivi mna zaidi ya CRDB Wakala 20,000 waliosambaa nchi nzima hususani vijijini. Hii itasaidia sana kuchochea shughuli za kibiashara katika maeneo ambayo mwanzo ilikuwa ni ngumu kufika kwa uwekezaji wa matawi,” aliongezea Bashungwa.

Bashungwa alisema pamoja na kuongezeka kwa huduma za benki kupitia uwakala, benki zinapaswa kutoa mafunzo kwa mawakala ili kuongeza weledi na kuboresha huduma kwa wateja. “Niwapongeze Benki ya CRDB kwa kuendesha semina hii ya kuwajengea uwezo mawakala. Niwasihi CRDB Wakala wote mliohudhuria hapa msikilize kwa umakini na kutoa huduma kama mafunzo yanavyoelekeza, weledi wenu katika kutoa huduma ni muhimu sana katika kuwahudumia Watanzania na kuboresha sekta ya fedha nchini,” alisema Bashungwa.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe aliipongeza Benki ya CRDB kwa kufikisha huduma za CRDB Wakala kwa wakulima kupitia vyama vya ushirika (AMCOS) na mawakala binafsi huku akibainisha kuwa jitihada hizo zimesaidia wakulima wengi nchini kufungua akaunti za Benki. 

“CRDB Wakala imesaidia kuwawezesha wakaulima kupokea malipo yao moja kwa moja kupitia akaunti zao za Benki, jambo ambalo limeondoa udanganyifu na dhuluma kwa wakulima,” alisema Bashe.


IMG-20200806-WA0023
Lusinga Sita Meneja wa Kanda ya Ziwa akitoa maelezo kwa Waziri Innocent Bushungwa alie ambatana na Naibu waziri wa Kilimo Hussein Bashe kwenye ufunguzi wa mafunzo ya CRDB Wakala yaliyotolewa na CRDB Benki Mkoani Simiyu.

Kwa upande wake Meneja wa Kanda ya Ziwa Benki ya CRDB, Lusing Sitta alimwambia Waziri wa Viwanda kuwa semina hizo zilizoandaliwa kwa ajili ya CRDB Wakala nchi nzima zinalenga katika kuboresha utoaji huduma kwa wateja na kuwajengea uwezo mawakala hao.

Sitta alisema CRDB Wakala wamekuwa na mchango mkubwa katika kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wateja kutokana na kusogeza hudma za benki karibu. “CRDB Wakala wanatoa huduma zote kuanzia kufungua akaunti, kuweka na kutoa pesa, malipo ya Ankara na malipo ya tozo na kodi za serikali,” alisema Sitta huku akibainisha kuwa mwaka jana pekee CRDB Wakala ilisaidia kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 300.

Sitta alimwambia Waziri Bashungwa kuwa Benki ya CRDB katika mkakati wake wa biashara wa miaka mitano imedhamiria kuongeza matumizi ya mifumo ya kidijitali kama CRDB Wakala, SimBanking, SimAccount na Internet Banking ili kusaidia kufikisha huduma za kifedha kwa watanzania wengi zaidi.

“Mwaka jana asilimia 86 ya miamala ya wateja wetu ilifanyika kupitia njia hizi za kidijitali,” alimalizia Sitta huku akisema mwaka huu Benki ya CRDB imejipanga kufanya semina hizo za CRDB Wakala katika wilaya 50 Tanzania.

IMG-20200806-WA0022
Baadhi ya CRDB Wakala wakifuatilia kwa makini mafunzo yanayo tolewa na Benki ya CRDB Wilayani Bariadi-Simiyu.

IMG-20200806-WA0027
Mkuu wa Wilaya ya Busega Bi. Tano Mwela akimkabidhi zawadi mmoja wa CRDB Wakala ambaye anafanya vizuri kwa kufungua akaunti nyingi zaidi kwa wastani wa akaunti 90 kwa siku.
IMG-20200806-WA0021 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com