Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Waziri Mkuu Akagua Ujenzi Wa Sgr Dar-ruvu......Asema Ameridhishwa Na Kasi Na Viwango Vya Mradi Huo

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa leo (Ijumaa, Agosti 7, 2020) amekagua ujenzi wa mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) na amesema kwamba ameridhishwa na kiwango na kasi ya maendeleo ya ujenzi huo ambao umefikia asilimia 87 kwa kipande cha kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro.

Amesema Serikali imedhamiria kuimarisha miundombinu ya usafiri wa reli, anga, maji na barabara ili kutoa fursa kwa wananchi kuchagua aina ya usafiri wanaohitaji kuutumia pia kukamilika kwa mradi huo kutaimarisha biashara baina ya Tanzania na Mataifa mengine.

Waziri Mkuu ambaye alianza ziara hiyo kwa kukagua ujenzi wa jengo la stesheni ya Dar es Salaama ambalo linamuonekano wa madini ya Tanzanite, amesema ujenzi unaendelea vizuri na amemtaka mkandarasi akamilishe kwa wakati kwani Watanzania wanasubiri kwa hamu. 

“Hii ni mara yangu ya tatu nafanya ukaguzi wa ujenzi wa mradi huu na wakati wote naridhishwa na maendeleo ya ujenzi wake ambao unajengwa kwa kutumia fedha za Watanzania na asilimia 90 ya wafanyakazi wanaojenga mradi huu ni Watanzania.”

Waziri Mkuu amesema Watanzania waendelee kuiamini Serikali yao kwa sababu imejipanga katika kuendelea na kuimarisha ujenzi wa miradi mbalimbali kwa ajili ya maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla.” Na huu ndio utekelezaji wa maelekezo ya CCM iliyoyatoa kwa Serikali yake.”

Akiwa katika stesheni ya Ruvu mkoani Pwani, Waziri Mkuu alipokea malalamiko mbalimbali kutoka kwa wananchi yakiwemo ya wakulima kunyanyaswa na wafugaji kwa kuingiza mifugo katika mashamba yao hivyo kuwafanya wakose chakula.

Pia, wananchi hao ambao baadhi yao maeneo yao yalitwaliwa kupisha ujenzi wa mradi wa SGR kwamba wamehamia kwenye maeneo ambayo hayana miundombinu ya maji. Kufuatia malalamiko hayo Waziri Mkuu amemuagiza Mkuu wa mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo kesho aende na wataalamu wake wakasikilize kero za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia Uchukuzi, Mhandisi Atashasta Nditiye  amesema mafanikio yanayoonekana katika mradi huo ni matokeo ya kazi kubwa inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli.

Amesema tayari mkandarasi anayejenga mradi huo kampuni ya Yapi Merkezi ameanza kufanya majaribio ya kupitisha treni za kihandisi katika baadhi ya vipande vya kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro. “Mchakato wa manunuzi ya seti tano za mabehewa ya abiria unaendelea.”

Mhandisi Nditiye amesema licha ya ujenzi wa mradi wa SGR pia shirika la Reli linatekeleza mradi wa uboreshaji wa Reli ya Kati kutoka Dar es Salaam hadi Isaka na maboresho hayo yamefikia asilimia 93 kwa kipande cha Dar es Salaam hadi Tabora na unatarajiwa kukamilia Februari 2021.

Awali, Mtendaji Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania, Bw. Masanja Kadogosa amesema ujenzi wa kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro unaendelea vizuri na umefikia asilimia 87. “Hadi sasa mkandarasi amelipwa jumla ya hati za malipo 34 sawa na sh. trilioni 1.7 kwa kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro. Mradi huo umetoa ajira zaidi ya 7,400 Dar es Salaam-Morogoro.

Amesema kazi ya ujenzi inayoendelea kwa kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro ni pamoja na ujenzi wa daraja kubwa lenye urefu wa kilimita 2.56, majengo ya stesheni za Dar es Salaam (85%), Pugu (99%), Soga (100%), Ruvu (95%), Ngerengere (93%), Morogoro (93%), eneo la karakana na mizigo Kwala (73%) na ujenzi wa madara 30 ambao umefikia (96%).

“Ujenzi wa tuta la reli umefikia asiliamia 91, ujenzi wa mfumo wa mawasiliano ukijumlisha ujenzi wa minara 28 ya mawasiliano umefikia asilimia 43, ujenzi wa umeme wa msongo kv 220 upo asilimia 99, ujenzi wa vivuko 55 vikiwemo 20 vya juu, 17 vya chini na 13 vya wanyama na vitano vya makutano ya reli ya SGR na MGR, ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 92.”

(Mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com