Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAZIRI MKUU AKAGUA UKARABATI WA MV NEW VICTORIA


WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amekagua ukarabati  mkubwa wa meli ya MV New Victoria Hapa Kazi tu na kuagiza mamlaka inayosimamia ihakikishe kuwa kuanzia wiki ijayo meli hiyo inaanza kazi ya kusafirisha abiria na mizigo kwa kuwa ukarabati umekamilika na sasa inaendelea kukaa tu  hali ambayo ni hasara kwa Serikali.

Pia, Waziri Mkuu ametoa siku mbili kwa mamlaka inayohusika na utoaji wa kibali cha kuanza kazi kwa meli hiyo ihakikishe inatoa kibali hicho haraka na  ratiba ya safari itangazwe kwa sababu  Watanzania wanahamu  ya kuanza kuhuduiwa na meli hiyo.

Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo leo (Jumapili, Agosti 9, 2020) baada ya kukagua meli hiyo ambayo tayari imeshafanya safari ya majaribio  kwa  kusafirisha  abiria kutoka Mwanza hadi Bukoba mkoani Kagera ambako ilirudi na abiria na mizigo.

Maeneo aliyokagua kwenye meli hiyo ni pamoja na vyumba vya abiria vikiwemo vyumba maalumu kwa ajili ya huduma za mama na mtoto, chumba cha kuongozea meli, vyumba vya migahawa na chumba cha injini.

“Nimeona ukarabati mkubwa uliofanywa, nimeona injini mpya, meli imekamilika na ilishafanyiwa majaribio ya aina zote kubeba abiria na kubeba mizigo na wataalamu wamejiridhisha kuwa inauwezo wa kubeba abiria na mizigo.”

Waziri Mkuu ameongeza kuwa “Haya yote ni mawazo na mipango ya Rais Dkt. John Magufuli pamoja na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya 2015-2020. Tumetekeleza na tunaendelea kutekeleza.”

Baada ya kukagua meli ya MV New Victoria Hapa Kazi Tu, Waziri Mkuu alikagua ujenzi wa chelezo pamoja na meli mpya na alieleza kuwa ameridhishwa na kazi inayoendelea kufanyika na amewataka Watanzania waendelee kuwa na imani na Serikali yao.

Awali, Meneja Miradi ya Kimkakati inayotekelezwa na Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) Luteni Kanali Vitus Mapunda alisema miradi hiyo minne ya ukarabati mkubwa wa meli ya Mv Victoria Hapa Kazi Tu, MV Butiama Hapa Kazi Tu, ujenzi wa chelezo na ujenzi wa meli mpya inayojulikana kama MV Mwanza Hapa Kazi Tu itagharimu sh. 152,916,249,842.

Alisema ukarabati wa meli ya MV New Victoria Hapa Kazi Tu yenye uwezo wa kubeba abiria 1,200 na mizigo tano 400 umegharimu sh. 22,712,098,200. Meli hiyo itatoa huduma ya usafirishaji wa abiria na mizigo kati ya bandari ya Mwanza Kaskazini, Kemendo na Bukoba.

“MV Butiama itakayobeba abiria 200 na mizigo tani 100 ukarabati wake umegharimu sh. 4,897,640,000. Meli hiyo itatoa huduma ya usafirishaji wa abiria na mizigo kati ya bandari ya Mwanza Kaskazini na Nansio Ukerewe. Ukarabati wa chelezo umegharimu sh. 36,152,511,642 na ujenzi wa meli mpya utagharimu sh. 89,154,000,000.”

Alisema kukamilika kwa miradi hiyo ya kimkakati kutafungua fursa nyingi za ajira binafsi na kupunguza gharama za usafirishaji sambamba na kuongeza tija katika shughuli za biashara hivyo kuwafanya wananchi wanyonge wengi kunufaika. Ujenzi wa Meli mpya unatarajiwa kukamilika Agosti 2021.

(Mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com