Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Mwingulu Nchemba amewataka watendaji wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kutekeleza majukumu yao kwa vitendo ikiwemo kusimamia mashauri mbalimbali kwa uweledi ili kuhakikisha haki inapatikana kwa ajili ya maslahi mapana ya Taifa.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam wakati akifanya ziara ya kikazi katika Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali Dkt. Nchemba, amesema kuwa hatapenda kuona uzembe unafanywa kwa mawakili wasomi wa serikali katika kusimamia haki.
"Mtendaji yoyote akifanya kosa ambalo litaleta madhara kwa taifa kupitia utendaji wake, atachukuliwa hatua za kisheria kuwa amehujumu uchumi” amesema Dkt. Nchemba.
Amesema kuwa ni vizuri mawakili kuacha kufanya kazi kwa mazoea, badala yake kuendelea kulinda rasilimali za taifa kwa wivu mkubwa ili kuokoa mali za watanzania katika kutafuta haki
Awali, Wakili Mkuu wa Serikali, Gabriel Malata. alimlalamikia Dk. Mwigulu kwamba kuna baadhi ya taasisi za umma hazitoi ushirikiano wakati wa uandaaji wa hati za utetezi katika kesi mbalimbali zikiwamo zenye maslahi ya nchi, hivyo kusababisha wapate ushindi au kushinda kwa taabu.
Akijibu, Dkt.Nchemba alitoa maagizo taasisi za umma zinazokataa kutoa ushirikiano kwa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali zichukuliwe hatua kama zinafanya kosa la uhujumu uchumi
"Inapotokea au itakapotokea taasisi zitakashindwa kutoa ushirikiano kwa makusudi na mara kwa mara, tuzijue na wachukuliwe kwamba, wanashiriki kuhujumu maslahi ya taifa,” alisema na kuongeza:
“Hii pia hata kwa mawakili wa serikali wanaotoa mwanya katika kuandaa kesi ili upande wa pili ushinde, lazima wafanyiwe assesment (tathmini) wasije kutuambia kwamba tumepigwa kitekiniko.”
Alisema vita ya kiuchumi hupiganiwa kisheria, kiakili, kimaandishi, hivyo yanapokuja maslahi ya nchi kuna upande mmoja tu kwao ambao ni ushindi.
"Vita ya kiuchumi haipiganiwi porini, hupiganiwa kwa kutumia akili na uwanja wa mapambano unakuwa sheria, mtu anabatilisha haki ya wengi kuwa ya yake binafsi, jukumu la kuingia katika vita ya kichumi ni sisi tuliokabidhiwa dhamana," alisema Dk. Mwigulu.
Aidha, aliitaka ofisi hiyo kuwa macho na kujipanga kuelekea kipindi cha uchaguzi kwa wale wanaotaka kupitisha mikono yao na watakaotaka kulipa fadhila za ‘mabwana zao’.