Aliyekuwa mfanyakazi (mwanahabari) wa ITV na Redio One, Agnes Almasy mapema leo ameagwa rasmi katika Kanisa la Anglikana la Mtakatifu Nichoulaus, Ilala jijini Dar es Salaam.
Mtangazaji huyo alipatwa na umauti Septemba 3 Buguruni Jijini Dar es Salaam alipokuwa akijiandaa kuelekea kazini na alifariki akiwa njiani kuelekea hospitali ya Amana jijini Dar es Salaam.
Misa hiyo ya kuaga ilihudhuriwa na viongozi wa IPP Media, wafanyakazi na watu mbalimbali wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa ITV/Radio One Joyce Mhaville.
''Agnes alikuwa mchapakazi mzuri sana, aliyependa kujifunza kila siku na alikuwa mchangamfu sana na mwenye kupenda kufurahi muda mwingi kwakweli tumepoteza mfanyakazi mahiri na aliyefanya kazi zake kwa ufanisi mkubwa", amesema Julieth Robert ambaye ni Mfanyakazi na msomaji habari wa ITV.
"Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa ajili ya maisha ya Agnes Almasy kwani sote tulitoka kwa Mwenyezi Mungu na kwake tutarejea'', ameongeza.
Baada ya Ibada ya kuaga mwili, marehemu anatarajiwa kusafirishwa kuelekea Mkoani Tanga ambapo atazikwa katika Makaburi ya Bombo. Agnes ameacha mume na mtoto mmoja na aliajiriwa rasmi kufanya kazi na ITV na Redio One Machi 19, 2018.
Via EATV