Katibu mkuu CCM Dr. Bashiru Ally
Na Azmala Said - Malunde 1 blog
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) akiwa njiani kuelekea Mwanza, ametoa maagizo kwa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa CCM kujibu hoja zote zinazotolewa na wagombea wa vyama vya upinzani zenye lengo la kupotosha watanzania.
Ameyasema hayo leo tarehe 6 Septemba, 2020 akizungumza na kamati ya utekelezaji ya vijana Mkoa wa Shinyanga.
"Kupitia kamati ya utekekelezaji ya Umoja wa Vijana mkoa wa Shinyanga naagiza kwa niaba ya umoja wa vijana nchi nzima kujibu hoja zote zinazotolewa na wapinzani kwa sababu majawabu tunayo, majawabu yapo katika kazi tulizofanya kwa miaka mitano, majawabu yapo katika historia ya Chama chetu, majawabu yapo katika uongozi wa Chama chetu, majawabu yapo katika sifa za wagombea wetu na uwezo wao, msikae kimya."
Katibu Mkuu amesisitiza kuwa, "Semeni kwenye redio, semeni kwenye mitandao, semeni kwenye mikutano ya hadhara, msiruhusu uongo kurudiwa marambili, hata hii habari ya kwamba watu waingie barabarani waelezeni kwamba hakuna watanzania wa zama hizi watakaoingia barabarani katika nchi yao huru katika miaka yao 60 ya uhuru, katika utulivu wa nchi hii, katika shibe tulionayo wanawapelekaje watu barabarani."
Aidha, Dkt. Bashiru ameongeza kuwa, "Muwakinge vijana wenzenu dhidi ya propaganda za uchochezi kwa kujibu hoja, na nataka moto huu wa kujibu hoja uanzie Shinyanga."
Mgombea wetu hawezi kujibu hoja za uongo, hilo ni jukumu la vijana.
"Kuanzia leo nitaanza kupima uimara wenu kwa kujibu hoja, uwezo mnao, uzoefu wa kutosha mnao, mmefundwa vya kutosha, mmelelewa, mmeandaliwa, sasa fanyeni kazi yenu",amesema.
Awali, Katibu Mkuu amepita ofisi ya CCM wilaya ya Nzega ambapo amefafanua kuwa:
"Hakuna Mgombea yeyote ndani ya Chama kutoka eneo lake la jimbo bila idhini ya kamati ya Siasa ya Wilaya, kwa hiyo kutokuwa na mpinzani ni nafuu ndogo, haiwaondolei mfumo wa kutokufuata ratiba za kamati za siasa za wilaya na NEC kwa kuwatafutia wagombea udiwani kura na Mgombea wetu Urais kura pamoja na kufafanua Ilani yetu kipi kimetekelezwa na kipi tunatarajia kutekeleza, pamoja na kuhamasisha wananchi kwenda kupiga kura."
"Nimemuona Nape Yupo Ilemela Mwanza, eti kwa sababu amepita bila kupingwa, huo ni utoro, kwenye mkoa wake wa Lindi Mhe. Kikwete anakwenda tarehe 8 kuzindua kampeni, anatakiwa awe kule kumuandalia mkutano, yeye yupo Ilemela. Katika hili tutakuwa wakali katika eneo la nidhamu, hatuwezi kuwa kama vyama vingine vinavyokusanyana wakati wa uchaguzi, wagombea wa CCM wapo chini ya kamati za siasa, waliomba wao wenyewe na lazima wafuate maelekezo ya kamati za siasa, sio wagombea binafsi." Katibu Mkuu ameonya.
Pia Katibu Mkuu amemuonya Mhe. Hamisi Kigwangala kuendekeza mabishano mitandaoni hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi badala ya kutumia mitandao ya kijamii kukitafutia chama ushindi,
"Mhe. Kigwangala naona anazunguka kwenye mitandao ya kijamii kujibizana na Mohammed Dewji mambo ya mipira, tupo kwenye uchaguzi, mi nataka nione ana tweet na wafuasi wake namna Mwenyekiti na Rais wetu atakavyoshinda, mwengine anaweza kuona naingilia maisha binafsi, hakuna maisha binafsi unapokuwa mgombea wa CCM, hilo mumueleze kabisa.",amesema Bashiru.
Katika kumkaribisha Katibu Mkuu, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Nzega Bw. Amosi Kanuda akiambatana na Mbunge wa jimbo La Nzega Mjini Mhe. Hussein Bashe pamoja na viongozi wengine, amemuhakikishia Katibu Mkuu ushindi wa kishindo kwa Chama Cha Mapinduzi kwa nafasi za Udiwani na Urais, ikumbukwe kuwa Wilaya ya Nzega ina majimbo matatu na mawili tayari wagombea wa CCM wamepita bila kupingwa.
Social Plugin