Aliyekuwa Mbunge Jimbo la Kishapu Suleiman Nchambi akimuombea kura Boniphace Butondo wakati wa uzinduzi wa kampeni za uchaguzi CCM Jimbo la Kishapu katika Kijiji cha Nhobola kata ya Talaga wilayani Kishapu - Picha na Suzy Luhende
Suzy Luhende, Shinyanga
Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kishapu Suleiman Nchambi amemuombea kura mgombea ubunge wa Jimbo hilo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Boniphace Butondo na kuahidi kushirikiana naye ili aweze kupata ushindi wa kishindo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni za Uchaguzi CCM za mgombea ubunge Boniphace Butondo, uliofanyika jana kijiji cha Nhobora kata ya Talaga wilayani Kishapu, Nchambi aliwaomba wananchi wote wa Jimbo la Kishapu kumpa kura zote Butondo ili aweze kushinda kwa kishindo.
Alisema amewatumikia wananchi kwa muda wa miaka 10 hivyo hana budi kukabidhi kijiti kwa Butondo ili aendeleze gurudumu la maendeleo katika wilaya ya Kishapu.
"Ndugu zangu Wana Kishapu nawashukuru sana kwa ushirikiano wenu mlionipatia wakati nikiwa mbunge kwa miaka 10, sasa naomba mmpe ushirikiano Butondo kwani sitaki kuona kura hata moja inaenda upinzani, zote tumpigie diwani wa kata hii mbunge wa Chama Cha mapinduzi pamoja na Rais John Pombe Magufuli",alisema Nchambi.
Alisema Jimbo la Kishapu halitabadilika kwa sababu aliyemwachia ni mchapakazi lakini litaongezeka kimaendeleo, kwa sababu anamjua vizuri, kwani wameshirikiana naye wakati akiwa mwenyekiti wa halmashauri hiyo kwa kufanya maendeleo ikiwemo kujenga barabara, na kutatua changamoto mbalimbali, hivyo anaamini ataendelea kufanya makubwa zaidi.
"Nimekuwa kimya kwa kipindi kirefu si kwamba nimezira naahidi kwamba nitashirikiana naye Butondo na kuhakikisha Chama Cha Mapinduzi kinachukua dola, na nitakuwa naye bega kwa bega na kushirikiana na CCM siku zote za maisha yangu,kwa sababu mmenitoa katika migongo yenu na mmenishauri mengi", alisema Nchambi.
Alisema atashirikiana na Viongozi wote wa Chama Cha Mapinduzi ili kuhakikisha Jimbo la Kishapu linapata kura nyingi za kutosha na kuhakikisha Kishapu inaongoza kwa kura nyingi kuanzia kwa madiwani mbunge na kwa Rais.
Kwa upande wake Mgombea ubunge Boniphace Butondo aliwaomba wananchi wote wa Kishapu wamchague ili aweze kuwatumikia kwani anajijua yeye ni mchapakazi mzuri katika kudimamia maendeleo.
Aliwaomba wananchi wa Jimbo hilo wakiamini Chama Cha Mapinduzi kwani kimefanya mambo makubwa yakiwemo ya sekta ya elimu,ambapo serikali kupitia Chama Cha Mapinduzi imejenga madarasa, imetengeneza madawati na kujenga nyumba za walimu.
Butondo alisema pia serikali kupitia Chama Cha Mapinduzi imejenga zahanati katika kata mbalimbali na vijiji na itaendelea kupanua vituo vya afya ili kina mama wenye matatizo mbalimbali yakiwemo ya upasuaji wahudumiwe ndani ya wilaya.
Aidha alisema akichaguliwa kuwa mbunge atahakikisha akina mama wanakopeshwa ile asilimia nne, vijana asilimia nne na walemavu asilimia mbili ili waweze kufanya biashara na kujikwamua kiuchumi.
"Tayari serikali kupitia Chama Cha Mapinduzi Jimbo la Kishapu kimeshatoa mikopo kwa vikundi saba ambavyo vinajishughulisha na ufugaji wa kuku na baadhi ya vijana wameshakopeshwa pikipiki kwa ajili ya kufanya boda boda ili kujipatia ridhiki",alieleza.
Alisema katika sekta ya maji, atahakikisha maji ya ziwa Victoria yanasambazwa katika kata zote za Kishapu, ikiwa Ni pamoja na huduma ya umeme kusambazwa vijiji vyote vya Jimbo hilo.
"Wapendwa wananchi wangu naomba sana mmpe kura zote Rais Magufuli na mmpe kura zote diwani wa kata hii na upande wa ubunge nipeni mimi ili niweze kuwaletea maendeleo kwa kushirikiana na Rais wangu mpendwa, mchapa kazi John Pombe Magufuli,"aliongeza Butondo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Mabala Mlolwa aliwaomba wananchi wanaochonganisha waache mara moja wamuache mbunge aliyemaliza muda wake ashirikiane na mbunge mteule wafanye kazi za chama kama timu.
Mgombea ubunge Jimbo la Kishapu mkoani Shinyanga kupitia Chama Cha Mapinduzi CCM Boniphace Butondo akiteta jambo na Mbunge aliyemaliza muda wake Suleiman Nchambi (kulia) kwenye uzinduzi wa kampeni ya ubunge Kishapu. Picha na Suzy Luhende
Mgombea Ubunge Jimbo la Kishapu Boniphace Butondo akicheza pamoja na waliokuwa watia nia ya kuwania ubunge Jimbo la Kishapu
Mgombea Ubunge Jimbo la Kishapu Boniphace Butondo akicheza pamoja na waliokuwa watia nia ya kuwania ubunge Jimbo la Kishapu
Mgombea ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi CCM, Boniphace Butondo akinadi sera zake na kuomba kura kwa wananchi wa Kishapu kwenye uzinduzi wa Kampeni za Uchaguzi katika Kijiji Cha Nhobola kata ya Talaga wilayani Kishapu
Mgombea Ubunge viti maalumu mkoa wa Shinyanga Lucy Mayenga akimuombea kura mgombea ubunge kupitia CCM Boniphace Butondo na madiwani pamoja na Rais John Pombe Magufuli
Mgombea Ubunge viti maalumu mkoa wa Shinyanga Lucy Mayenga akimuombea kura mgombea ubunge kupitia CCM Boniphace Butondo na madiwani pamoja na Rais John Pombe Magufuli
Mwenyekiti wa chama Cha Mapinduzi CCM wilaya ya Shinyanga Shija Ntelezu kulia akiwa na Viongozi wenzake wakicheza kwenye uzinduzi wa kampeni za CCM