Na Dinna Maningo,Rorya.
Aliyekuwa mgombea ubunge jimbo la Rorya mkoani Mara kupitia chama cha Mapinduzi (CCM) Lameck Airo, mfanyabiashara maarufu Ongujo Wakibara na waliokuwa wagombea nafasi ya ubunge wa jimbo na viti maalumu wameungana pamoja kumuombea kura Jafari Chege aliyeteuliwa kugombea ubunge.
Makada hao walimuombea kura Rais Magufuli, Chege na Madiwani wa CCM jana wakati wa uzinduzi wa kampeni za mgombea Udiwani kata ya Goribe Ogaja Mbega aliyemaliza muda wake na anatetea kiti hicho cha Udiwani.
Airo alisema kuwa katika uongozi wake wa miaka 10 ya ubunge amefanya maendeleo hususani katika sekta ya elimu na kupambana kudhibiti wizi wa mifugo na masuala mbalimbali ya kijamii.
"Ni mengi ya kueleza ambayo nimeyafanya,pamoja na elimu yangu ndogo ya darasa la saba lakini nimejitahidi kadri ya uwezo wangu,kwasababu leo ni uzinduzi sitaongea sana tutakutana kwenye kampeni zinazoendelea, nyie ni mashahidi mnajua mchango wangu katika maendeleo,nilitumia hata pesa zangu za mfukoni bila kuisahau Serikali ya Chama Cha Mapinduzi amefanya mengi", alisema Airo.
Airo aliongeza kuwa wizi wa mifugo umepungua ikilinganishwa na miaka iliyopita kabla ya uongozi wake hivyo aliwaomba wananchi kumchagua Chege ili aendeleze pale alipoishia.
Aliongeza" elimu yangu ni ya darasa la saba lakini pamoja na kwamba sijasoma nimefanya maendeleo kadri ya uwezo wangu,watu wanasema nimeacha ubunge wizi utaanza, Chege ataendeleza",alisema Airo.
Mfanyabiashara maarufu mkazi wa Shirati Ongujo Wakibara alisema kuwa kuna baadhi ya watu wamekuwa wakieneza maneno kuwa Tarafa ya Nyancha haiwezi kumpigia kura Jafari jambo alilolikanusha.
"Eti wanasema Nyancha haiwezi kumpa Jafari huo ni uongo kura tutampa Jafari tunaomba wana Tarafa ya Girango tuungane pamoja tuipigie kura CCM tumpe kura Jafari mimi ndiyo mzee wa mafuta hakishindikani kitu, tutashinda", alisema Ongujo.
Waliotia nia nafasi ya ubunge viti maalumu Stella Odatt na Joyce Oming'o waliwaomba wananchi wa Goribe kutowaangusha hususani akina mama na kusema kuwa CCM ndiyo chama pekee kinacholeta maendeleo kwa wananchi.
Waliotia nia kugombea ubunge wa jimbo hilo akiwemo Wambura Sasi alisema kuwa wapo kwa kazi moja ya kumnadi Jafari Chege huku Dkt. Patrick Makabelo aliyekuwa mtia nia jimbo la Kawe mkoani Dar es Salaam akisema kuwa Airo amefanya mambo mazuri yanayoonekana na kwamba watakuwa bega kwa bega kumwombea kura Jafari.
Frederic Magadi alisema .."Serikali ya awamu ya tano imefanya mambo mengi tunayaona msidanganyike mabadiliko yoyote yale yanaletwa na Chama cha Mapinduzi wakati wenyewe wanafanya migomo CCM inasonga mbele".
Obuya Osogo alisema kuwa yeye anamuunga Chege akitokea Tarafa ya Nyancha 'Tunahitaji mbunge atakayetuletea maendeleo na huyo ni Jafari".
Leonard Otuoma alisema kuwa licha ya kwamba yeye ni kijana mdogo hakuogopa kugombea na kwamba baada ya kura kutotosha anaungana na Chege na kazi yake ni kunadi Chama cha Mapinduzi.
Francis Olwero alisema.."Nilipogombea nilikuwa na mawili kushinda au kushindwa,nimeshindwa sasa namuunga Jafari,Chadema wamenipigia sana simu kuwa nisimuunge mkono Jafari Chege watia nia tumepigiwa simu sana nasema nitakaa hapa hapa Rorya Dar nitaenda nikiwa na matokeo ya ushindi wa Jafari",alisema Olwero.
Waliotia nia ya Udiwani kata ya Goribe na kura kutotosha walimuunga mkono mgombea Udiwani na kusema watakuwa pamoja kumwombea kura Ogaja.
Kenedy Seda alisema kuwa kutia nia siyo uadui kwakuwaCCM ina Demokrasia na ilifanya uteuzi na kumchagua Ogaja.
Osoro Silisi alisema kuwa uchaguzi ni mchakato kila mtu ana haki ya kugombea kwa kuwa kura zake hazikutosha anamuunga mgombea aliyeshinda huku Philemon Diambe akiwashukuru wananchi kwa kura walizompa na kusema kuwa hana kinyongo na kwamba wanaosema hamuungi Ogaja hao ni wazushi na wachonganishi.
Uzinduzi huo ulihudhuriwa na mgombea Udiwani kata ya Roche Jumanne Oketto na wagombea wengine wanaotetea kiti cha Udiwani ambao wamemaliza muda wao wa miaka mitano na kuteuliwa tena kugombea walimwombea kura Ogaja.
Wagombea hao ni Willium Mamba wa kata ya Bukura,Charles Chacha kata ya Nyamtinga, aliyekuwa mwenyekiti wa CHADEMA wilaya ya Rorya na Diwani wa kata ya Kirogo Jastin Rogoye na kutimkia CCM na Deogratus Ndege kutoka kata ya Bumera wilaya ya Tarime.
"Kata yangu iko jirani na Rorya tumesaidiana Airo kuwafuchua wezi wa mifugo na sasa wizi umepungua,John Heche tangu awe mbunge hajawahi kuisaidia kata yangu lakini Airo alinipa saruji mifuko 100 na mabati 100 kuisaidia kata, naombeni mpeni kura Ogaja ili tuendelee kukomesha wizi", alisema Ndege.
Mgombea Udiwani kata ya Goribe Ogaja Mbega aliwaomba wananchi wake kuichagua CCM na yeye mwenyewe na kwamba wizi wa mifugo ndiyo ulisababisha agombee udiwani na mafanikio yameonekana.
Hata hivyo baada ya uzinduzi huo timu hiyo inayompigia kampeni Chege waliongozana hadi nyumbani kwa Airo na kisha kufanya tathmini ya kampeni na kupanga mikakati ya kampeni kuhakikisha CCM inashinda.
Mgombea Ubunge Jimbo hilo Jafari Chege aliwashukuru watia nia kwa kuonyesha ushirikiano kumuunga mkono na kusema kuwa ushirikiano huo umempa furaha na matumaini ya ushindi.
Wananchi wa kata ya Goribe wakiwa kwenye uzinduzi wa mgombea Udiwani kupitia CCM kata ya Goribe Ogaja Mbega
Mfanyabiashara Ongujo Wakibara akizungumza
Wanawake wa Goribe wakiimba wimbo
Aliyekuwa mtiania wa Ubunge ambaye kura hazikutosha Wambura Sasi akizungumza
Wananchi wakicheza ngoma ya Ritungu
Obuya Osogo akizungumza
Wagombea wa Udiwani viti maalumu
Patrick Makabelo aliyekuwa akitia nia Ubunge jimbo la Kawe-Dar es Salaam
Mtiania Ubunge Rorya Fedrick Magadi
Mtiania Ubunge Leonard Otuoma
Aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA wilaya ya Rorya na Diwani wa kata ya Kirogo Jastin Rogoye aliyetimkia CCM na kuteuliwa kugombea udiwani
Wananchi wa Goribe wakicheza ngoma ya asili
Wana CCM na wananchi wakicheza
Ogaja Mbega mgombea Udiwani kata ya Goribe