Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa
Na Faustine Gimu Galafoni,Dodoma.
WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye tamasha la "Karibu Dodoma "linalotarajiwa kufanyika Oktoba 22-24 Jijini Dodoma.
Akizungumza na waandishi wa habari Hayo leo Jijini Dodoma na Mratibu wa tamasha hilo Saimon Mwapagata (Rado) amesema Lengo la tamasha hilo ni kupongeza juhudi za Rais John Magufuli katika kukuza na kutangaza mkoa na Jiji la Dodoma ikiwa ni sehemu za kuendeleza fikra za baba wa Taifa juu ya makao makuu kuhamia Dodoma.
Mwapagata amesema tamasha hilo 'Karibu Dodoma Festival 'litakuwa na maudhui ya kutoa fursa kwa makundi mbalimbali ya jamii na kwenye sekta mbalimbali ambazo zimefanya vizuri na kuleta mabadiliko chanya kwa jamii.
"Tunatumia Jiji la Dodoma katika kuratibu mambo makubwa yanayo unganisha Taifa kwa sababu Dodoma ndio makao makuu ya nchi ,"amesema.
Amebainisha kuwa katika kutoa fursa ilivyokusudiwa makundi ya jamii pamoja na sekta mbalimbali zitapewa nafasi ya kutoa ushuhuda wa mabadiliko yanayofanywa na Serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi wa Dk. John Magufuli.
"Tunapaswa kutoa shukrani zetu kwa Serikali ya awamu ya tano,na katika kufanya hivyo Kuna baadhi ya makundi yaliyopata mabadiliko ya ushindi ndani ya miaka makundi hayo yatapata nafasi ya kueleza ushindi huo;
Amesema makundi hayo ni pamoja na bodaboda,mama ntilie,machinga,watu Wenye ulemavu ,wanafunzi wa vyuo ,vijana,wanawake na Wazee.
Hata hivyo amesema kuwa tamasha hilo halipo kisiasa na kwamba Wananchi wanapaswa kutofautisha tamasha hilo na nguvu ya siasa .
Kwa upande wake Katibu wa Jumuiya ya watu wenye ulemavu Tanzania John Mlabu amesema ,kundi hilo linatambua mchango wa Serikali ya awamu ya tano hivyo kwa nguvu moja wameamua kuunga mkono tamasha hilo.
"Tumeshuhudia Rais akiwajali walemavu kwa vitendo ,jamii ilizoea kuona walemavu wakiwa ombaomba ,maisha yao yalikuwa magumu,lakini Sasa hali imebadilika tuna nafasi ya kufanya biashara na kujijenga kiuchumi,"amesema.
Naye mwakilishi wa wanawake wajasiriamali Jijini Dodoma Mariam Fentu ameeleza kuwa ni Wakati wa kuyaweka hadharani mambo waliyifanyiwa na Serikali ya Magufuli ambapo alisema imewashika mkono kwa asilimia 99.
"Tukimkopesha Magufuli kura zetu na Sasa anatulipa maendeleo kwa vitendo,tunafanya biashara kwa mikopo nafuu ya asilimia 4 iliyotolewa na Serikali kwa kundi la wanawake"amesema.