Mgombea ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi CCM Jimbo la Shinyanga Mjini,Patrobas Katambi akiwa kwenye mkutano wa hadhara katika kata ya Mwamalili manispaa ya Shinyanga. Picha na Suzy Luhende.
Mgombea ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi CCM Jimbo la Shinyanga Mjini,Patrobas Katambi akiwa kwenye mkutano wa hadhara katika kata ya Mwamalili manispaa ya Shinyanga.
Mgombea udiwani kata ya Mwamalili manispaa ya Shinyanga Paul Machela akiomba kura kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata hiyo na kuhudhuriwa na mgombea ubunge Jimbo la Shinyanga Mjini Patrobas Katambi.
Mgombea ubunge viti maalumu kupitia Chama Cha Mapinduzi mkoa wa Shinyanga Christna Mzava akiwa kwenye mkutano wa hadhara katika kata ya Mwamalili manispaa ya Shinyanga akiomba kura za diwani, mbunge na Rais wa Chama Cha Mapinduzi CCM.
***
Na Suzy Luhende - Shinyanga
Mgombea Ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Patrobas Katambi ameendelea na Kampeni zake Uchaguzi ambapo leo alikuwa katika kata ya Mwamalili ambapo amewaomba wananchi wamchague ili aweze kuwatua ndoo kichwani akina mama kwa kuwatengenezea mtandao mkubwa wa maji ya kisima.
Hayo aliyasema leo wakati akizungumza kwenye mkutano wa hadhara katika kata ya Mwamalili, ambapo aliwaomba wananchi wa kata hiyo wamchague kwa kura zote ili aweze kuwatua ndoo kichwani akina mama na kuleta maendeleo mbalimbali katika kata hiyo.
Katambi pia aliwaomba wananchi hao kumchagua John Pombe Magufuli na diwani wa Kata hiyo Paul Machela ambaye atawakilisha kero mbalimbali zilizopo na kuweza kutatuliwa.
"Najua kuna changamoto nyingi katika kata hii zikiwemo za kilimo, nichagueni mimi na Rais Magufuli ili tuweze kuwaletea matrekta ya kulimia ambayo tutayaleta kwenye kata na mengine ya kuwakopesha",alisema Katambi.
Alisema katika sekta ya uchumi na biashara wataangalia ni namna gani kaina mama waweze kujikwamua kiuchumi wakiwemo vijana wote,hivyo wataleta wataalamu ambao watawafundisha akina mama kutengeneza batiki na vitu vingine vya kimaendeleo.
Pia aliwaomba wazee wamuamini waunde Baraza la Wazee ambalo litakuwa na viongozi litawasilisha kero zote zilizopo katika kata na zitafanyiwa kazi kwa wakati zikishindikana zitapelekwa bungeni na wazee watapata haki zao.
Kwa upande wake mgombea udiwani wa kata hiyo Paul Machela alisema kuna kero ya daraja la kwenda Old Shinyanga daraja litaanza kujengwa na zahanati ya kijiji cha Bushola imekamilika, zahanati ya Mwamalili nayo imekamilika na wanajenga maabara ikiisha tu tayari itaanza kutumika.
"Mimi ndiye diwani niliyekuwepo nawaambia ukweli, na sasa nagombea ili tumalizie yaliyobaki, hivyo kila kitu kitakamilika ndani ya uongozi wa Chama Cha Mapinduzi na kwa kufuata Ilani ya Chama Cha Mapinduzi CCM",alisema Machela.
"Niseme ukweli wa Machela alianza udiwani Mwaka 1995 enzi za Mkapa mpaka sasa anaendelea kusimamia miradi mbalimbali zikiwemo zahanati,maji ya ziwa Victoria na maendeleo mengi mbalimbali",alisema Kampeni Meneja wa diwani Paul Machela, Fulushi Matinde.