KIKOYO AANIKA VIPAUMBELE SITA AKICHAGULIWA KUWA MBUNGE MULEBA

Mgombea ubunge Jimbo la Muleba Kusini Dk. Oscar Kikoyo

Na Ashura Jumapili - Muleba
Mgombea Ubunge Jimbo la Muleba Kusini Dr.  Oscar Kikoyo ametaja vipaumbele sita vitakavyopewa msukumo baada ya kuchaguliwa kuongoza Jimbo hilo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa shule za kidato cha tano na sita.


Akihutubia wananchi waliofurika katika uwanja wa Red cross mjini Muleba, Dr Kikoyo alisema Sera ya elimu bure inayotolewa na Serikali ya awamu ya tano imeibua mahitaji mbalimbali baada ya ongezeko la wanafunzi wanaosajiliwa kwenye shule za msingi na sekondari.

Alisema pamoja na suala la ujenzi wa vyumba vya madarasa kuendelea, pia nguvu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali itaelekezwa kwenye ujenzi wa shule za kidato cha tamo na sita katika maeneo tofauti ya Jimbo hilo.

Akitaja maeneo mengine kuwa ni ujenzi wa visima vidogo vya maji kama sehemu ya mwendelezo wa kazi iliyoanza miaka mitano iliyopita ya kumtua mama ndoo kichwani kwa kusogeza karibu huduma za maji

Vipaumbele vingine ni Afya kwa kujenga na kuboresha zahanati na vituo vya afya na miundombinu ya barabara na kuwahaidi wananchi uwakilishi shirikishi na kuimarisha mipango ya kuongeza makusanyo kutoka vyanzo mbalimbali ili yatumike kuchochea maendeleo ya wananchi.

Mbunge wa zamani wa Jimbo hilo ambaye hakugombea tena nafasi hiyo Profesa Anna Tibaijuka alisema kwa kumpata Dr. Oscar Kikoyo anaamini analiacha katika mikono salama na kuwa katika uongozi wake ametoa mchango mkubwa katika maeneo tofauti.

Katika mkutano huo aliyekuwa Mwenezi wa Wilaya kupitia Chadema Kassim Mustafa alirejea CCM akisema kuwa anaunga.mkono kazi iliyofanyika kwa miaka mitano iliyopita na kuwa yuko rayari kushirikiana na wagombea waliopitishwa na CCM kutafuta kura na kushirikiana nao kutafuta maendeleo ya Jimbo hilo.

Aidha mkutano ulihudhuriwa na mgombea Ubunge wa Muleba Kaskazini Charles Mwijage aliyesema kasi ya maendeleo katika Wilaya hiyo itaongezeka zaidi na kuwaomba wananchi kuwachagua ili wasimamie utekelezaji wa ilani ya chama hicho.

Dr. Kikoyo ni Mwanasheria na wakili wa kujitegemea ambapo pia ni Mhadhiri wa muda katika vyuo vikuu tofauti nchini  na  ametumikia nyadhifa tofauti za uongozi Serikalini.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post