Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimetembelea kituo cha kulea watoto yatima cha Mama wa Huruma kilichopo Madale, Dar es Salaam.
LHRC wamefanya tukio hilo la kiutu Ijumaa, Septemba 11, 2020 ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 25 tangu kuanzishwa kwake (LHRC).
Akizungumza na wanahabari, mwakilishi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Bi. Naemy Sillayo amesema LHRC wameamua kutembelea kituo cha kulea watoto kama sehemu ya muendelezo wa kupaza sauti kukemea ukiukwaji wa haki za watoto na kuisihi jamii kuongeza ulinzi kwa watoto.
“Kwetu sisi (LHRC) hii si mara ya kwanza kutembelea vituo hivi vya kulea watoto wanaoishi katika mazingira magumu, tunafanya hivi kwa kuwa moja ya kazi yetu kubwa ni kuhamasisha ulinzi wa haki za watoto hapa nchini. Tunaposheherekea miaka 25 tangu kuanzishwa kwa LHRC tunaendelea kuonesha kwamba tunaguswa sana na ukiukwaji wa aina yoyote ile wa haki za watoto na pia tunachukua hatua kuhakikisha haki za watoto zinalindwa",amesema.
Sillayo ameongeza kwamba kupitia hatua hiyo, LHRC wanaitaka jamii ichukue hatua kuongeza ulinzi kwa watoto ili kuhakikisha watoto wanafurahia haki zao na hatimaye kuifikia jamii yenye haki na usawa.
“Katika kuadhimisha miaka 25 kama jamii kwa ujumka tunapaswa kuongeza ulinzi kwa watoto, tuongeze ulinzi kwa watoto bila kujali ni mtoto wako wa kumzaa au ni mtoto wa mwingine. Kila mmoja akitimiza wajibu wake tutapunguza ukatili dhidi ya watoto.” ameongeza Sillayo.
Kwa upande wa kituo cha Mama wa Huruma, mwakilishi wa kituo hicho, Sista Christina Christopher amesema walianzisha kituo hicho baada ya kuguswa na hali mbaya ya maisha waliyokuwa nayo watoto yatima na watoto wanaoishi katika mazingira magumu na kuamua kuwasaidia.
“Mara kwa mara tulikuwa tukipita katika mitaa mbalimbali tuliwaona watoto wakiteseka kwa kukosa malazi na huduma za msingi, wengine walishinda njaa, wengine wazazi wao walishindwa kuwasaidia, hii ilitugusa sana na kuamua kuanzisha kituo hiki ili kuwasaidia”,amesema Sista Christina.
Sista Christina pia amekipongeza Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kwa kufika na kutoa msaada katika kituo hicho cha Mama wa Huruma.
Kituo cha kulea watoto cha Mama Huruma kilianzishwa mwaka 2010 kwa lengo la kuwasaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu kupata haki za msingi ikiwemo haki ya kupata malazi, haki ya elimu, haki ya afya na haki ya kupata ulinzi. Tangu kuanzishwa kwa kituo cha Mama wa Huruma, kituo hicho kimesaidia watoto wengi yatima na wanaoishi katika mazingira magumu kupata hifadhi na kupata malazi na huduma nyingine za msingi kama elimu.
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinaadhimisha miaka 25 ifikapo Septemba 26 mwaka 2020. Shirika hilo la utetezi wa haki za binadamu lilianzishwa Septemba 26 mwaka 1995 kwa lengo la kusimamia misingi ya haki, usawa, utawala wa sheria, demokrasia na utawala bora nchini Tanzania. Kilele cha maadhimisho ya miaka 25 ya LHRC kitafanyika Septemba 25 jijini Dar es Salaam.
Social Plugin