Mgeni rasmi katika uzinduzi wa kampeni ya ubunge kwa CCM Jimbo la Isimani, MNEC wa mkoa wa Iringa ambaye pia ni Mratibu wa Kampeni wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Salim Abri (ASAS) akimnadi mgombea ubunge jimbo la Ismani, William Lukuvi
Mgeni rasmi katika uzinduzi wa kampeni ya ubunge kwa CCM Jimbo la Isimani, MNEC wa mkoa wa Iringa ambaye pia ni Mratibu wa Kampeni wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Salim Abri (ASAS) akivalishwa skafu na vijana wa CCM kumkaribisha kwenye uzinduzi wa kampeni jimbo la Kalenga.
Mgeni rasmi katika uzinduzi wa kampeni ya ubunge kwa CCM Jimbo la Isimani, MNEC wa mkoa wa Iringa ambaye pia ni Mratibu wa Kampeni wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Salim Abri (ASAS) akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni jimbo la Ismani
Msanii Harmonize akiwa na furaha baada ya kumaliza kuimba katika uzinduzi wa kampeni jimbo la Ismani kwa tiketi ya CCM.
Na Denis Mlowe - Iringa
Mgombea Ubunge wa jimbo la Ismani lililoko Iringa Vijini mkoni Iringa ambaye pia ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) William Lukuvi amezindua kampeni kuwania nafasi hiyo huku akiwataka wananchi katika ukanda wa Isimani kuwachagua tena viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kura za kishindo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliofanyika katika kijiji cha Migoli, Lukuvi alisema kuwa chini ya uongozi wa awamu ya tano iliyo chini ya Rais John Pombe Magufuli serikali imefanikiwa kuleta mafanikio makubwa ya kimaendeleo ikiwemo kumaliza kero ya uhaba wa maji kwenye maeneo hayo ambayo ilikuwa changamoto kubwa.
Alisema kuwa serikali ya CCM imedhamiria kwa kiasi kikubwa kumalizia utekelezaji wa miradi michache ya maendeleo iliyobakia katika jimbo hilo endapo itapata tena ridhaa kutoka kwa wananchi.
Alisema kuwa kwa kipindi cha miaka mitano wakazi wa jimbo la Ismani wameshuhudia kwa kiasi kikubwa miradi ambayo serikali imefanya hivyo miradi ambayo haijakamilika ikiwemo vituo vya afya atahakikisha vinamaliziwa miaka mitano ijayo.
Lukuvi alisema kwa sasa miradi iliyobaki anahifahamu na atahakikisha sekta ya elimu inakuwa kwa kuwajengea mabweni wanafunzi ili wanaokaa mbali iwe rahisi kwao kusoma hivyo wasihadaike na wanaojipitisha kuomba kura.
Aidha aliwaomba wananchi wa jimbo la Ismani kuhakikisha wanamchagua kwa kura za kishindo mgombea urais wa CCM, John Magufuli na madiwani ili maendeleo yafike kwa kasi kama miaka mitano iliyopita.
Alisema wamchague mgombea udiwani wa kata ya Migoli ili kurahisisha mawasiliano ya kuwaletea maendeleo na kuachana na wagombea ambao hata namba zake hawana.
Naye Mgeni rasmi katika uzinduzi wa kampeni ya ubunge kwa CCM Jimbo la Isimani, MNEC wa mkoa wa Iringa ambaye pia ni Mratibu wa Kampeni wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Salim Abri (ASAS) alisema wakati umefika sasa wananchi kuzibia masikio wanasiasa wasio na mlengo na dhamira njema kwa Taifa ambao wapo tayari kuliingiza Taifa katika machafuko ili mradi tu wapate kura.
Aliwataka kumpigia kura za kishindo kwani kazi ambazo amefanya nchini kila mmoja anatambua hivyo ni wakati sahihi wa kumwongezea miaka mitano kuweza kuikamilisha ahadi ambazo amekuwa akizitoa na kuzikamilisha kwa wakati.
“Nani asiyejua kwamba Rais Magufuli kafanya makubwa kwa nchi yetu ambaapo kwa miaka mitano tu kafanya mengi ambayo kama wengekuwa marais wengine wangefanya miradi ya maendeleo kwa kipindi cha miaka kumi na tano hivyo mpeni kura Rais John Magufuli”, alisema.
Alisema kuwa wakazi wa Ismani wasiache kumpigia kura mgombea ubunge wa jimbo hilo, Williama Lukuvi ambaye maendeleoa aliyowafanyia jimbo hilo ni makubwa hivyo anahitaji miaka mingine mitano kuweza kuikamilisha miradi iliyobaki.
Uzinduzi huo ambao ulipambwa na wagombea ubunge wa majimbo mengine na wenyeviti wa usalama wa wilaya msanii wa muziki wa bongo fleva, Harmonize ulifana kwa kuhudhuriwa na maelfu ya wakazi wa jimbo la Ismani.