Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WANAODAIWA KUWA MAJAMBAZI WAUAWA KWA KUPIGWA MAWE WALIPOVAMIA DUKA LA M-PESA KAHAMA MJINI


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Watu wawili wanaodaiwa kuwa ni Majambazi wameuawa kwa kupigwa mawe na wananchi baada ya majambazi hao kuvamia duka la M-Pesa na kufyatua baruti hewani kisha kumshambulia kwa kumpiga mabapa ya panga mmiliki wa kibanda cha M-Pesa na kupora shilingi milioni 1.7 Mjini Kahama mkoani Shinyanga. 

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari leo Septemba 9,2020, Kamanda wa Polisi mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba amesema tukio hilo limetokea Septemba 8,2020 majira ya saa mbili na nusu usiku katika eneo la Manzese, Kata ya Busoka, Tarafa ya Kahama mjini, wilaya ya Kahama na mkoa wa shinyanga. 

“Majambazi wawili ambao bado hawajafahamika majina wala makazi yao, umri kati ya miaka 25-30, waliuawa kwa kurushiwa mawe na wananchi wa eneo la Manzese Mjini Kahama baada ya majambazi hao kuvamia duka la M-pesa na kufyatua baruti hewani kisha kumshambulia kwa kumpiga mabapa ya panga mgongoni mmiliki wa kibanda cha M-pesa aitwaye Paulo Charles Inena (32), mfanyabiashara mkazi wa Lugela kwa lengo la kumnyang'anya pesa za mauzo”,ameeleza Kamanda Magiligimba. 

“Majambazi hao walifankiwa kunyang'anya shilingi 1,750,000/=.

Majambazi hao walijaza baruti kwenye maganda yaliyotumika na kuyalipua kwa kutumia silaha aina ya shortgun”  ameongeza Kamanda Magiligimba. 

Kamanda Magiligimba amefafanua kuwa, wananchi waliokuwa eneo hilo walifanikiwa kuwarushia mawe majambazi hao sehemu mbalimbali za miili yao na kusababisha mauaji hayo. 

Amesema kuwa Miili ya marehemu imehifadhiwa katika hospitali ya halmashauri mji wa Kahama kwa utambuzi. 

“Kwenye eneo la tukio hilo ilipatikana silaha moja aina ya shortgun ambayo imekatwa kitako na mtutu, maganda matatu ya short gun yaliyotumika kujazia baruti, vocha tisa za halotel za tsh.1000/= na tano za tsh.500/=, vocha saba za Vodacom za tsh.1000/= na saba za tsh. 500/=, vocha saba za Airtel za shilingi 1000/= na simu moja aina ya Tecno”,amesema. 

Kamanda Magiligimba anatoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Jeshi la polisi kutoa taarifa mara tu wanapobaini viashiria vyovyote vya uhalifu, ili kukabiliana na matukio ya uhalifu na wahalifu kabla ya uhalifu kutokea.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com