Sada Mkumba akionesha mtandao wa Bayogesi jikoni kwake
Sada Mkumba akionesha mtandao wa Bayogesi jikoni kwake
Na Joyce Joliga - Songea
Kwa muda mrefu wananchi wengi wamekuwa wakiumiza kichwa namna ya kupata fedha za kuingiza umeme kwenye majumba yao na wengine wakijikuta wakikosa pesa za kununua nishati ya umeme au mkaa hivyo kujikuta familia zao zikiwa na maisha magumu.
Lakini hali hiyo ni tofauti kabisa kwa Sada Mkumba ambaye muda wote amekuwa ni Mama mwenye furaha na anayejiamini.
Siri kubwa ya kujiamini kwa Sada maarufu Mama Nyanzi Mkazi wa Mateka B Manispaa ya Songea inaelezwa imetokana na kuwa na uhakika wa kuweza kuandaa chakula cha familia yake kutokana na kufanikiwa kuweza kutumia Bayogesi inayotokana na kinyesi cha ng'ombe.
Tayari Mwanamama huyo amejizolea umaarufu mkubwa kwa majirani zake kutokana na kuweza kubuni mradi wa kutumia kinyesi cha Ng’ombe kwa ajili ya matumizi ya nyumbani ikiwemo kupikia,kuwasha taa pamoja na kuchaji simu.
Sada anasema, haikuwa kazi rahisi kwake kubuni mradi huo,ila alijikuta akilazimika kuanza kutumia bayogesi baada ya kuona anatumia fedha nyingi kununua mkaa na umeme ambapo kwa mwezi alijikuta akitumia zaidi ya sh 60,000 kutokana na kuwa na familia kubwa.
Anasema, baada ya kufuga kwa muda mrefu alijikuta akitamani kutumia bayogesi hivyo alishauriana na mumewe na wakakubaliana kutafuta mtaalamu ambaye aliwaelekeza na kuwachimbia shimo la wastani ambalo ndiyo walikuwa wakilitumia kuhifadhi na kukoroga bayogesi hiyo.
Anasema,Bayogesi anayotumia ni ya Kinyesi kilaini cha Ngo’mbe kisicho changanyika na uchafu wa majani amapo utumia ndoo mbili za maji na ndoo ya maji lita 20 kisha unakoroga kwenye kisima hadi inakuwa laini kisha unaweka kwenye mtandao wa shimo ambapo wamevitega vibomba ambavyo vinaingia kwenye mtandao wako.
“Kadri unavyoweka Samadi ndiyo unapata gesi nyingi unaweza kuchaji simu, taa na hata kupika pia ni rahisi sana kutumia na inapunguza matumizi ya mkaa , gharama zipo kwenye ujengaji wa shimo kulingana na size ya shimo",anasema Sada.
"Nimeitumia vizuri sana na nimepata mafanikio makubwa kwani kinyesi cha ngombe kizuri ambacho hakijachangangikana na nyasi ili kisiweze kujiziba joto kali ndiyo linasaidia kutoa gesi,” anaeleza.
Aidha, anataja faida bayogesi ya ng'ombe kuwa hailipuki na haina madhara yoyote hata chakula ukipikia kinaiva vizuri na hakiwi na harufu yoyote ,ni kama gesi asilia tu.
Anawashauri wanawake wawe na hamu ya kufuga ng'ombe ili waweze kupata mtandao huo kwani kuna faida kubwa sana wataipata wanaweza kupunguza bajeti zisizo za lazima pia kutunza mazingira kwa kutokata miti ovyo kwa ajili ya kuchoma mkaa,pia wataweza kupunguza matumizi ya umeme na mkaa.
Naye Emmanuel Kinunda mtaalam wa Bayogesi anasema ni rahisi sana kutumia kinyesi cha ng'ombe kama nishati ambapo amesema kwa muda mrefu amekuwa akitumia kinyesi cha ng'ombe kuweza kupikia chakula na ameweza kufanikiwa kupunguza gharama za mkaa na umeme ambapo awali alilazimika kutumia sh 25,00/= kwa mwezi kwa ajili ya kununua umeme na sh 40,000/= kwa ajili ya kununua mkaa ila sasa pesa hiyo inatumika kufanya vitu vingine vya maendeleo.
Anawataka wananchi kutumia nishati mbadala ili kuweza kuondokana na gharama za kununua umeme na mkaa pia wataweza kutunza mazingira yao na kuondoaa na uharibifu wa mazingira.
Social Plugin