KATIBU MKUU WIZARA YA ELIMU AWATAKA MAFUNDI SIMU KUWA WAAMINIFU

 Na Faustine Gimu Galafoni,Dodoma 
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia  Dkt.Leonard Akwilapo amewataka mafundi wa simu za mikononi kote nchini kuwa waaminifu pindi wanapotengeneza simu za wateja wao.


Dkt.Akwilapo amesema hayo leo Septemba 4,2020 jijini Dodoma katika hafla ya uzinduzi wa mafunzo ya umahiri ya ufundi wa simu za mkononi iliyofanyika ukumbi wa VETA.

Dkt.Akwilapo amebainisha kuwa asilima kubwa ya mafundi simu waliojifunza mtaani huharibu badala ya kutengeneza simu za wateja wao hivyo sehemu ya mafunzo hayo yatakuwa na chachu kubwa katika kufuata maadili na ueledi wa taaluma hiyo.

Aidha,Dkt.Akwilapo amesema zaidi ya asilimia 65% ya watanzania  wanatumia simu za mkononi ambapo Mwaka 2012 watumiaji walikuwa milioni 27 lakini wameongezeka hadi milioni 48 hadi sasa.

Katika hatua nyingine katibu Mkuu huyo Wizara ya Elimu ametoa wito kwa taasisi zingine kushirikiana na VETA katika kuwezesha mafunzo ya mafundi simu  huku akiwaasa wanufaika mafunzo kutoishia kwenye mafunzo na vyeti bali wawe chachu ya kuboresha huduma .

Mkurugenzi mkuu wa VETA Mhandisi Pancras Bujulu amesema mafunzo hayo yanalenga usalama wa simu za mkononi na kuongeza tija ya uchumi  huku mkuu wa chuo cha Teknolojia Dar es Salaam(DIT)  Prof. Prilesedis Ndomba akisema kuwa DIT imejipambanua kuwa taasisi ya Elimu ya juu katika Teknolojia na kuwaasa kusoma kwa bidii.

Katibu mkuu Baraza la ujuzi Tanzania  Edgar Job amesema vijana wanatakiwa kujitambua kuwa Tanzania inakwenda kwa kasi katika Teknolojia  na simu ni zaidi ya chombo cha Mawasiliano  huku mkurugenzi mkuu wa Tume ya TEHAMA Tanzania  Samson John Mwela   akibainisha kuwa uchumi wa dunia wa sasa  unategemea sana TEHAMA na kuwataka vijana kutumia fursa zinazotolewa na Serikali.

Mkurugenzi wa leseni na ufuatiliaji kutoka mamlaka ya Mawasiliano Tanzania(TCRA) John Daffa amesema kutokana na ukuaji wa huduma ya Mawasiliano TCRA ilibaini changamoto 13  ikiwa ni pamoja na kuongezeka vifaa holela na feki vya mawasiliano  hivyo mamlaka hiyo iliamua kuanzisha umoja wa mafundi simu ambao utakuwa unatambulika kisheria  na zaidi ya mafundi simu 185 walihitimu ukanda wa Dar es salaam na mafundi simu 160 Mwanza

Mkuu wa wilaya ya Dodoma Mjini Josephat Maganga kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Dkt Binilith Mahenge amesema  mafunzo hayo yanasaidia vijana kujiajiri wenyewe 

Mwenyekiti mafundi simu mkoani Dodoma Emmanuel Msangi amesema kuna mafundi simu zaidi ya 200 mkoani Dodoma waliopata mafunzo lengo ni kupanua wigo wa ajira kwa vijana huku Mwenyekiti wa mafundi simu Kanda ya Ziwa  Maguha Manyanda  Butonyole akisema kuanzishwa kwa Chama cha mafundi simu kumebadilisha Maisha yao .




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post