Chama cha Waaandishi wa Habari Wanawake TAMWA-Zanzibar chenye lengo la kuhakikisha udhalilishaji wanawake na watoto unamalizika Zanzibar kimewapa mafunzo ya kupambana na matendo hayo wanajamii wapatao 1972 katika mkoa wa Kaskazini Unguja.
Mafunzo hayo yamewanufainsha wanajamii wa makundi mbalimbali kutoka shehia tofauti ndani ya mkoa huo kwa kutumia wanamtandao maalumu ambao wamewezeshwa na Chama hicho katika utowaji wa elimu dhidi ya udhalilishaji kwa wanawake na watoto.
Akizungumza katika uwasilishwaji wa taarifa baada ya kufanyika wa mafunzo hayo, Afisa ufuatiliaji na tathmini kutoka TAMWA-Zanzibar Mohamed Khatib alisema utolewaji wa mafunzo hayo kwa jamii unalenga kuionesha jamii madhara ya udhalilishaji kwa watoto ambapo anaamini kuwa jamii isipokuwa na uelewa hwenda matendo hayo yakaendelea kusalia siku hadi siku.
Alisema wameamua kutoa elimu hiyo kwa idadi kubwa ya watu kutoka katika makundi mbali mbali ambayo yamekua katika mazingira hatarishi pia na kuna ulazima wa kupatiwa elimu hiyo.
Hata hivyo Afisa huyo alisema kuwa miongoni mwa wanufaika wa mafunzo hayo ni pamoja na wanafunzi waliopo vyuoni ikiwemo Chuo cha Amali Mkokotoni pamoja na kambi za JKU ambapo kwa kiasi kikubwa wanaonekana kuwa katika mazingira hatarishi kufuatia mchanganyiko wao na jamii tofauti.
Pamoja na hayo Afisa huyo aliwataka wanamtandao wa kupambana na udhalilishaji wa kijinsia mkoa wa kaskazini Unguja kuhakikisha wanafanya kazi zao bila ya kuchoka kwa maslahi ya jamii dhidi ya matendo hayo maovu.
‘’Ni lazima muwe na utaratibu wa kuitazama jamii kwa jicho la mbali na ikiwezekana elimu iliotolewa iwafikie wengi zaidi hata wale wasiokuepo kwenye mikutano yetu’’aliongezea.
Akiwasilisha ripoti ya utafiti mdogo uliofanywa na wanamtandao huo wa kaskazini Unguja Bi Kamu Vuai Khamis alisema zipo changamoto mbali mbali ambazo zinaendelea kuwakabili katika kupambana na vita ya udhalilishaji.
Alitaja changamoto hizo ni pamoja na baadhi ya wanajamii kutokua tayari kutoa mashirikiano kwa wanamtandao kwa lengo la kuibua kesi za udhalilishaji ambazo miongoni mwao ni watoto wao wanaofanyiwa.
‘’Kwa mfano hivi sasa katika moja ya Shehia mkoa wa Kaskazini Unguja mama mtoto amediriki kuficha taarifa za mtoto wake aliebakwa na kuamua kumpa dawa za kiswahili akiamini anaweza kupoa na hadi sasa bado mtoto huyo anaedelea na maumivu’’,alisema.
Akizungumzia kuhusu hali halisi ilivyo dhidi ya matukio hayo ya udhalilishaji alisema kwa kipindi cha miezi miwili iliopita jumla ya kesi nane zimeripotiwa huku saba kati ya hizo zinaendelea na ufuatiliaji na moja imeibuliwa kwa hatua ya awali.
Kwa upande wake Bi Hadia Ali Makame kutoka mkoa wa Kaskazini Unguja ambaye pia ni miongoni mwa wanamtandao wa kupinga matendo ya udhalilishaji alisema licha ya elimu kubwa inayoendelea kutolewa lakini bado kuna changamoto ikiwemo muitikio mdogo kwa baadhi ya wanajamii.
Mjumbe wa mtandao wa kupingana na udhalilishaji Mkoa wa kaskazini Unguja Kamu Vuai Khamis akiwasilisha ripoti fupi baada ya kufanyika kwa mafunzo ya kupambana na matukio ya udhalilishaji katika mkoa wa Kaskazini Unguja.
Social Plugin