Na Mwandishi wetu
MGOMBEA ubunge wa Jimbo la Nanyamba mkoani mtwara kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Abdallah Chikota, amezindua kampeni zake huku akitaja mambo zaidi ya matano atakayoyafanya endapo wakimchagua kuwa Mbunge.
Akizungumza leo kwenye uzinduzi wa kampeni za CCM, uliofanyika kwenye Kata ya Mtiniko Jimboni humo, Chikota ametaja mambo hayo kuwa ni kuboresha sekta ya afya kwa kuongeza vituo vya afya, zahanati kwenye maeneo ambayo hayana na kukamilisha ujenzi wa majengo yaliyobaki kwenye ujenzi wa Hospitali ya wilaya ambao ulishaanza.
Kuhusu sekta ya maji, Mgombea huyo amesema atahakikisha anasimamia ukamilishaji wa mradi wa maji ulioanza wa Nanyamba na Chawi.
“Nitahakikisha nafuatilia serikalini kuhusu uanzishaji wa mradi wa maji mkubwa ili kusaidia kata tano ambazo zina shida kubwa ya maji ikiwemo Mnima, Nyundo, Timbwilimbwi, Njengwa na Nitekela,”amesema.
Akizungumzia sekta ya elimu, ameahidi kuendelea kuboresha sekta ya elimu kwa kuboresha miundombinu ya shule kwa kujenga madarasa, nyumba za walimu na matundu ya vyoo,”amesema.
Kadhalika, amesema atahakikisha anasimamia serikali kukamilisha vijiji 52 ambavyo vimebaki bado havijapata umeme.
“Naomba mnichague tena kwa kipindi kingine cha miaka mitano, pia mchague Rais John Magufuli na wagombea wote wa CCM na madiwani wa kata zote 17, ili kuharakisha maendeleo ya Nanyamba, na katika miaka mitano iliyopita mmeshuhudia mafanikio mengi kwenye sekta mbalimbali, miaka mitano ijayo pia nitasimamia serikali kuongeza fedha zinazotengwa kwa aajili ya TARURA kukamilisha miradi ya barabara vijijini na kuweka lami kwenye vilima korofi,”amesema.
Katika mkutano huo wa kampeni, Mgombea huyo ametaja mafanikio mbalimbali yaliyopatikana kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita kuwa ni ujenzi wa hospitali ya wilaya iliyogharimu zaidi ya Sh.Bilioni 1, ujenzi wa vituo vya afya vitatu vya Majengo,Dinyecha na Kilomba vilivyogharimu
Sh.Bilioni 1.4.
“Kuna ujenzi wa zahanati 11 unaendelea, lakini pia halmashauri imepata magari matatu ikiwemo gari moja la mganga mkuu na mengine ya wagojwa (Ambulance),”amesema.
Pia, Mgombea huyo amesema wananchi wamebnufaika na ujenzi wa barabara ya Mtwara-Mnivata kwa kiwango cha lami unaoendelea na barabara za mzunguko za ndani katika halmashauri ambapo kila mwaka zinajengwa kilometa mbili kwa kiwango cha lami hivyo kufikia kilometa 11 .8 huku Shirika la mawasiliano hapa nchini (TTCL) ikijenga minara 11 ya simu.
“Kwahiyo ndugu zangu mnaona dhahiri mafanikio na faida inayofanywa na CCM tusifanye makosa mara mbili tufanye maamuzi sahihi tuchague Chama cha Mapinduzi ili tuzidi kunufaika na Maendeleo katika halmashauri yetu na mkoa kwa ujumla,"amesema Chikota.
Naye, Mgombea ubunge CCM Jimbo la Newala mjini Kapteni mstaafu George Mkuchika, amesisitiza kuwa "Tupige kura nyingi kwa CCM kwani uchaguzi uliopita CCM tulipoteza majimbo matatu ya uchaguzi ikiwemo Mtwara mjini, Ndanda na Tandahimba pamoja na Kata 62 kwahiyo msichague mtu ambaye hana serikali chagueni mtu mwenye serikali."
Kwa upande wake, Mgombea ubunge wa Jimbo la Tandahimba CCM, Ahmad Katani amewaomba wananchi Mkoani Mtwara kuchagua wagombea wa CCM ili kupata maendeleo ya kweli na kwa haraka ambapo kwa miaka mitano ijayo CCM itaendeleza kasi iliyoianza.
Social Plugin