BENKI YA CRDB YABORESHA HUDUMA KWA WASTAAFU WASTAAFU SASA KUHUDUMIWA KIDIJITALI

 

Afisa Mkuu wa Biashara wa Benki ya CRDB, Dkt. Joseph Witts (watatu kushoto) akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa mpango wa uwezeshaji kwa wastaafu uliyofanyika katika hoteli ya Golden Tulip jijini Dar es Salaam, leo. Wengine pichani ni kutoka kulia ni Mwenyekiti wa makatibu Wakuu Wastaafu, Michael Mwanda, Balozi Mstaafu Salome Sijaona, Mkurugenzi wa Wateja Wadogo na Wakati wa Benki ya CRDB, Boma Raballa, Mwenyekiti wa Umoja wa Polisi Wastaafu, Kamishna wa Polisi Mstaafu Suleiman Kova na Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi Benki ya CRDB, Adili Stephen.

Afisa Mkuu wa Biashara wa Benki ya CRDB, Dkt. Joseph Witts (watatu kushoto) akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa mpango wa uwezeshaji kwa wastaafu uliyofanyika katika hoteli ya Golden Tulip jijini Dar es Salaam, leo.  Kulia ni Mkurugenzi wa Wateja Wadogo na Wakati wa Benki ya CRDB, Boma Raballa na kushoto ni Mwenyekiti wa Umoja wa Polisi Wastaafu, Kamishna wa Polisi Mstaafu Suleiman Kova.

Benki ya CRDB imezindua mpango maalum wa uwezeshaji kwa wastaafu ambao unatoa fursa mbalimbali zinazolenga katika kuboresha maisha yao. Akizungumza katika uzinduzi wa mpango huo wenye kauli mbiu ya “Ndoto zako hazistaafu”, Afisa Biashara Mkuu wa Benki ya CRDB, Dkt. Joseph Witts amesema mpango huo anajumuisha fursa za kujiwekea akiba, uwekezaji, pamoja na uwezeshaji wa kifedha kwa wastaafu.

Dkt. Witts alisema pamoja na uzinduzi wa mpango huo Benki ya CRDB pia imezindua huduma za akaunti maalum ya wastaafu “Pension Account” na huduma ya uwezeshaji kifedha kwa wastaafu kidijitali “Pension Advance” kupitia huduma ya SimBanking App.

Akielezea kuhusu akaunti ya wastaafu, Dkt. Witts alisema akaunti hiyo inawawezesha wastaafu kupokea pensheni zao kwa urahisi na usalama na kujiwekea akiba kutokana na vipato vinavyotokana na shughuli mbalimbali za kiuchumi wanazozifanya. Dkt. Witts alisema ili kutoa nafuu kwa wastaafu akaunti hiyo hufunguliwa bure, haina makato yoyote yale na hutoa fursa kwa wastaafu kuunganishwa bure na mifumo ya utoaji huduma kidijitalli ikiwamo SimBanking na Internet Banking. 

“Ninajivunia kuwajulisha kuwa hadi leo hii tukiwa tunazindua mpango huu wa uwezeshaji wastafu, tayari wastaafu zaidi ya 19,000 wameshafungua akaunti hii na wanafurahia huduma zetu,” alisema Dkt. Witts huku akibainisha kuwa kupitia akaunti hiyo wastaafu wanapewa TemboCard inayowawezesha kupata huduma kwa CRDB Wakala na ATM zote nchi nzima.

Kwa upande wa huduma ya uwezeshaji wa kifedha kupitia “Pension Advance”, Dkt. Witts alisema sasa hivi wastaafu wanaweza kupata uwezeshaji wa fedha za kujikimu na kuendesha maisha yao kuanzia shilingi 50,000 hadi shilingi milioni 1 popote pale walipo kidijitali kupitia SimBanking App, huku akibainisha kuwa mkopo huo wa Pension Advance unatolewa bila riba yoyote.

Akizungumzia kuhusu fursa za uwekezaji zinazotolewa na Benki ya CRDB kupitia mpango huo, Dkt. Witts alisema benki hiyo pia imeanzisha akaunti maalum ya uwekezaji ijulikanayo kama “Akaunti ya Thamani” ambayo inawawezesha wastaafu kujipatia kipato kila mwezi. “Akaunti hii ya Thamani inatoa fursa kwa wastaafu kuwekeza kwa kipindi cha miaka mitatu kwa riba ya hadi asilimia 8,” alisema Dkt. Witts.

Naye Mkurugenzi wa Wateja Wadogo na Wakati wa Benki ya CRDB, Boma Rabala alisema kupitia mpango huo wa uwezeshaji kwa wastaafu benki hiyo pia imejipanga kuendelea kutoa mikopo kwa wastaafu ili kuwawezesha kuendeleza biashara na miradi yao ya maendeleo na hivyo kupunguza ukali wa maisha ya kila siku. Kupitia mkopo huo Wastaafu wanaweza kukopa kuanzia shilingi milioni 1 hadi shilingi milioni 100 kwa kipindi cha mwaka 1 hadi 7.

Mwenyekiti wa Makatibu Wakuu Wastaafu, Michael Mwanda aliishukuru Benki ya CRDB kwa kuwakumbuka wastaafu kupitia huduma na bidhaa zinazotolewa na benki hiyo. Mwanda alitoa rai kwa wastaafu wote kuchangamkia fursa hizo kuboresha maisha yao huku akiitaka Benki ya CRDB kutoa semina juu ya huduma hizo kwa wastaafu wote nchi nzima.

Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Polisi Wastaafu, Kamishna wa Polisi Mstaafu, Suleiman Kova aliipongeza Benki ya CRDB kwa kuja na mpango huo wa uwezeshaji kwa wastaafu huku akibainisha kuwa zitasaidia kuleta chachu ya maendeleo na kufanya kustaafu kusiogopwe. “Na sisi wastaafu sasa tunajidai tuna benki yetu ambayo sio tu inausikiliza bali pia inatambua mchango wa wastaafu katika taifa letu, Asanteni sana Benki ya CRDB,” alisema Kova huku akimuomba Afisa Biashara Mkuu wa Benki ya CRDB, Dkt. Joseph Witts kumsaidia kufungua akaunti ya Wastaafu ili aweze kufurahia huduma zote zinazotolewa katika mpango huo wa uwezeshaji wastaafu.









Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post