C –FM DODOMA YAPAZA SAUTI KUPINGA UKEKETAJI

Balozi wa ''Nisitiri nina haki ya kutimiza ndoto zangu,Usinikekete na usinipe Mimba Utotoni'' Msanii wa Muziki wa kizazi kipya Diana Exavery maarufu kwa jina la Malaika,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kutokomeza ukeketaji kwa Mikoa ya Kanda ya Kati inayoratibiwa na Redio hiyo iliyofanyika leo jijini Dodoma

Msimamizi Mkuu wa vipindi vya Redio ya C-FM,Emmanuel Likuda,akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kutokomeza ukeketaji kwa Mikoa ya Kanda ya Kati inayoratibiwa na Redio hiyo iliyofanyika leo jijini Dodoma

Balozi wa ''Nisitiri nina haki ya kutimiza ndoto zangu,Usinikekete na usinipe Mimba Utotoni'' Msanii wa Muziki wa kizazi kipya Diana Exavery maarufu kwa jina la Malaika,akiwa katika picha ya pamoja na Msimamizi Mkuu wa vipindi vya Redio ya C-FM,Emmanuel Likuda mara baada ya kuzindua kampeni ya kutokomeza ukeketaji kwa Mikoa ya Kanda ya Kati inayoratibiwa na Redio hiyo iliyofanyika leo jijini Dodoma.

...........................................................................................

Na. Alex Sonna, Dodoma

Kituo cha Redio C FM Mkoani Dodoma kimezindua Kampeni ya ''Nisitiri nina haki ya kutimiza ndoto zangu,usinikekete,usinipe mimba utotoni'' kwa mtoto wa kike ili waweze kutimiza ndoto zao.

kampeni hiyo imezinduliwa leo Jijini Dodoma kwa lengo la kutokomeza ukeketaji kwa Mikoa ya Kanda ya Kati inayoratibiwa na Redio ya C-FM ya jijini Dodoma na Msimamizi Mkuu wa vipindi wa Redio hiyo,Emmanuel Likuda .

Likuda ameeleza kuwa kwa mujibu wa ripoti ya Tanzania Demographic and Health Survey and Malaria (TDHS) kwa mwaka 2015-2016 inaonesha Mkoa wa Manyara unaongoza kwa kukeketa wasichana huku ripoti hiyo ikieleza kuwa wasichana wanaozaliwa au kulelewa na mama aliyekeketwa hukeketwa pia.

“hali ya ukeketaji nchini inaonesha kuwa Mkoa wa Manyara unaongoza kwa ukeketaji kwa asilimia 58 ukifuatiwa na Dodoma kwa asilimia 47,Arusha asilimia 41,Mara 32 na Singida asilimia 31”, ameeleza Likuda.

Aidha Likuda amesema kuwa ripoti hiyo imefafanua kuwa ukeketaji hufanywa kwa asilimia 86 na mangariba au wakeketaji wa jadi na asilimia 25 hukeketwa katika umri wa miaka 13 na zaidi.

Vile vile Ripoti hiyo imeeleza kuwa wasichana wanaozaliwa au kulelewa na mama aliyekeketwa hukeketwa pia na kuwa na asilimia 95 ya asilimia 86 ya wanawake waliokeketwa hawakubaliani na kitendo hicho na wanatamani kisiwepo kabisa

Naye Balozi wa kampeni hiyo Msanii wa Muziki wa kizazi kipya Diana Exavery maarufu kwa jina la Malaika, amesema madhara ya ukeketaji ni makubwa kiafya kwa mtoto wa kike ikiwemo kupata athari za kisaikolojia kama msongo wa mawazo kwani wengi hufanya hivyo bila ridhaa yao.

Pia Balozi huyo ameongeza kuwa Madhara ya afya ya uzazi ambayo hupelekea kuongezeka kwa vifo vya mama na mtoto wakati wa kujifungua pia maumivu makali wakati wa kukeketwa,kumwaga damu nyingi,kovu la kudumu sehemu za siri pamoja na kutokufurahia tendo la ndoa.

Kutokwa na damu nyingi,kovu la kudumu sehemu za siri pamoja na kutokufurahia tendo la ndoa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post