Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi pamoja na Kamishina ustawi wa jamii Naftari Ng'ondi wakikabidhi zawadi kwa wazee hao.
Na Ismail Luhamba, Manyoni Singida.
Katika kuelekea maadhimisho ya siku ya kimataifa ya Wazee, Oktoba Mosi, Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi ametembelea makazi ya Wazee mkoani Singida yaliyopo Sukamahela Wilayani Manyoni na kuzungumza nao ambapo amesema jamii ina kila sababu ya kuwatunza, kuwaenzi na kuwahudumia Wazee ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango wao katika Ustawi wa Jamii.
Akizungumza na Wazee hao juzi kwenye makazi hayo Dkt Nchimbi alisema Wazee ni tunu kwa taifa,kwani mawazo yao ndiyo yanayopelekea mafanikio makubwa ya taifa.
Alisema kupitia serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Dkt. John Pombe Magufuli imejikita kuimarisha uchumi kwa lengo la kuwasaidia wananchi wakiwemo Wazee ndio maana serikali ilianzisha makazi kwa ajili ya Wazee ili iweze kuwatunza.
"Tarehe 01 Oktoba ni siku ya wazee Duniani, siku hii ikatukumbushe kuwatunza wazee wetu.Familia zetu tuwatunze Wazee wetu,kama unachangamoto ya kumtunza mzeee wako nenda kwa Viongozi wako,nenda kwa Mkuu wa Wilaya toa taarifa ili serikali iweze kukusaidia" ,alisema Dkt Nchimbi.
Aidha aliwakabidhi zawadi mbalimbali ikiwemo mafuta ya kula,mchele,ndoo za maji, Sukari,mbuzi mnyama,Nyama na sabuni huku akiwaambia Wazee hao kuwa serikali inatoa matibabu bure kwao,hivyo kama kuna baadhi ya madaktari kwenye Zahanati,Vituo vya afya na Hospitali za Mkoa huo hawatekelezi jambo hilo watoe taarifa ili kutatua changamoto hiyo ikiwemo kuchukua hatua za kisheria.
"Serikali inawapenda sana ndiyo maana mpo na hapa tumeona imefanya ukarabati wa majengo yetu,tunahitaji mawazo kutoka kwenu ili na sisi tufike hapo mlipo", alisema Dkt Nchimbi.
Awali akisoma taarifa ya Wizara ya afya maendeleo ya jamii jinsia Wazee na watoto kwa niaba ya katibu mkuu wa Wizara hiyo Naftari Ng'ondi Kamishina ustawi wa jamii alisema mpaka sasa serikali inatoa matunzo kwa wazee 281 katika makazi 13 ya wazee nchini ambapo eneo la Sukamahe ni moja ya makazi hayo.
"Hapa Sukamahe tunatunza jumla ya wazee 15, Wizara inajivunia kupata mafanikio katika maeneo mbalimbali ya utoaji huduma kwa wazee tunaowahudumia hapa nchini", alisema Ng'ondi.
Alisema serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya majengo ya makazi ya wazee kwa kufanya ukarabati wa majengo yaliopo na kuanzisha majengo mapya ambapo kwenye makazi ya Sukamahe serikali imejenga jengo la utawala kwa lengo la kuimarisha mazingira mazuri ya kazi kwa watumishi wa makazi hayo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa makazi ya Sukamahe Andrea Yohana aliishukuru serikali kwa kuendelea kuwajali na kuwatunza wazee,na kuiomba serikali isichoke kuwatunza licha ya kuwa hawana uwezo wowote wa kuilipa.
"Tunaliombea taifa letu liweze kuvuka salama kwenye kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi kama alivyotuvusha kipindi cha Corona ili tuendelee kuishi kwa amani." alisema mzee huyo.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi akihutubia wazee wa makazi ya Sukamahe.
Wazee wa makazi ya Sukamahe wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Singida.
Wazee wa makazi ya Sukamahe wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Singida.
Jengo jipya la utawala lililopo kwenye makazi ya Sukamahe
Social Plugin