Mkurugenzi
Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) Abdul-Razaq
Badru (katikati) akizungumza na waandishi wa vyombo vya habari Agosti 31 mwaka
huu kuhusu kuongezwa kwa muda katika dirisha la maombi ya mikopo kwa wanafunzi
wa elimu ya juu katika mwaka wa masomo 2020/21. Kushoto ni Meneja Masoko wa
Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) Joseph Kimaro na kulia ni Meneja Mkuu
Uendeshaji Biashara wa Shirika la Posta Tanzania (TPC) Mwanaisha Said.
*******
TAARIFA KWA UMMA
KUFUNGWA KWA MAOMBI YA MIKOPO KWA MWAKA 2020/2021
1.0 UTANGULIZI
Tunafahamisha
wadau wote kuwa kuwa leo Alhamisi
(Septemba 10, 2020) saa 6:00 usiku dirisha la upokeaji wa maombi ya mikopo
kwa wanafunzi wa elimu ya juu kwa mwaka wa masomo 2020/2021 kwa njia ya mtandao,
litafungwa rasmi. Baada ya muda huo,
usajili mpya kwa ajili ya maombi
mapya hautaruhusiwa.
2.0
MUDA WA UOMBAJI KWA NJIA YA MTANDAO
Tarehe 21 Julai, mwaka huu, HESLB ilifungua
dirisha la maombi ya mkopo kwa njia ya mtandao na kisha kufuatia maombi ya
wazazi, walezi na wanafunzi, muda wa maombi ya mkopo uliongezwa kwa siku 10
hadi leo Septemba 10, 2020 saa sita
usiku. Mpaka mchana wa leo, jumla ya maombi 92,947 yamesajiliwa na kupokelewa yakiwemo maombi 7,500 yaliyopo katika hatua mbalimbali
za ukamilishwaji.
HESLB inatoa wito kwa waombaji mikopo 7,500 wenye maombi yasiyokuwa na viambatisho muhimu, kukamilisha maombi hayo haraka
iwezekanvyo ili yaweze kujumishwa kwenye tathmini na uchambuzi.
3.0
DIRISHA LA UHAKIKI WA MAOMBI KWA WAOMBAJI MIKOPO
Uhakiki wa taarifa za maombi ya mikopo, utaanza tarehe 1 Oktoba na kisha HESLB itaorodhesha maombi yaliyobainika kuwa
na kasoro mbalimbali kupitia katika mfumo.
4.0 WITO KWA WADAU WA HESLB
Kwa
kuzingatia kuwa mchakato wa maombi ya mikopo unahusisha wadau mbalimbali, HESLB
inawasisitiza wadau inaoshirikiana nao ikiwemo Shirika la Posta Tanzania (TPC)
kuendelea kuwahudumia waombaji mikopo wote kwa kupokea na kutuma maombi yao kwa
kuzingatia mwongozo wa uombaji mikopo kwa mwaka wa masomo 2020/2021.
6.0 BAJETI KWA MWAKA WA MASOMO
Serikali
kupitia HESLB, imetenga kiasi cha TZS
Bilioni 464 kwa ajili ya wanafunzi 145,000,
ambapo kati yao wanafunzi wanufaika 54,000
watakuwa wa mwaka wa kwanza na 91,000
ni wanafunzi wanufaika wanaoendelea na masomo.
7.0 HITIMISHO
HESLB
inawashauri wazazi, walezi na wanafunzi kuendelea kufuatilia vyanzo rasmi
ikiwemo tovuti ya HESLB (www.heslb.go.tz)
kuhusu taarifa muhimu na orodha ya watakaopangiwa mikopo kwa mwaka wa masomo 2020/2021 na kwa mujibu wa kalenda ya mwaka
wa kitaaluma (academic almanac) ya mwaka huu.
Imetolewa na:
Abdul-Razaq Badru,
Mkurugenzi Mtendaji,
10 Septemba, 2020,
DAR ES SALAAM.