MAJALIWA: AWAMU YA TANO IMEIPAISHA SEKTA YA MADINI


MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali itahakikisha mapinduzi makubwa yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli katika sekta ya madini yanaendelezwa.


Aliyasema hayo jana jioni (Ijumaa, Septemba 4, 2020) kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara baada ya kumuombea kura Rais Dkt. John Pombe Magufuli na mgombea ubunge wa Jimbo la Simanjiro, Christopher Ole Sendeka na wagombea udiwani.

“Tunaomba mumpe ridhaa Rais Dkt. Magufuli ya kuongoza awamu nyingine ili aweze kuendelea kushirikiana nanyi kufanya mambo makubwa katika kuboresha sekta ya madini. Sekta hii ameiimarisha sana na sasa dunia nzima inajua kwamba madini ya Tanzanite yanatoka Tanzania.”

Alisema Serikali itahakikisha inaendelea kuwawezesha wananchi kuwa sehemu ya umiliki wa rasilimali hiyo ya madini na CCM itahakikisha sekta ya madini inachangia zaidi katika pato la Taifa na kupunguza umasikini nchini.

Alisema miongoni mwa mapinduzi makubwa yaliyofanywa na Rais Dkt. Magufuli katika sekta ya madini ni pamoja na uboreshwaji wa miundombinu muhimu katika maeneo ya migodi na uchimbaji kwa kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo ujenzi wa ukuta unaozunguka migodi ya Mirerani na kuimarisha udhibiti wa madini ya Tanzanite, hivyo kuongeza tija kwa wachimbaji na Taifa kwa ujumla.

Alisema katika kuhakikisha wachimbaji wa madini wanaendelea kunufaika, Serikali imejenga masoko ya madini 28 nchi nzima ambapo mchimbaji mdogo ana fursa ya kwenda kuuza na kupata fedha ya kutosha ukilinganisha na miaka ya nyuma. "Ukienda dukani na madini yako unauza unapata pesa."

Kwa upande wao wakazi wa eneo la Mirerani hususani wachimbaji wadogo wa madini wamempongeza Rais Dkt. Magufuli kwa uamuzi wake wa kujenga ukuta mkubwa kwenye machimbo ya Tanzanite katika eneo la Mirerani kwa sababu ukuta huo umekuwa na manufaa makubwa kwao.

Walisema ukuta wa Mirerani umewezesha idadi kubwa ya vijana wanaofanya biashara ya madini kunufaika na shughuli hiyo na hali zao za Maisha zimebadilika tofauti na awali. “Tunampongeza Rais wetu Dkt. Magufuli sasa tuna maisha bora kutokana na uamuzi wake wa kujenga ukuta hapa Mirerani.”

Saning’o Ole Lengoje ni miongoni mwa vijana walionufaika na maboresho yaliyofanyika katika sekta ya madini ambapo alisema zamani kabla ya ujenzi wa ukuta huo watu wachache sana walinufaika, hivyo aliwaomba vijana wenzake waiunge mkono Serikali ya CCM kwa sababu inawajali wanyonge.

Awali, Waziri Mkuu alifanya mkutano wa kampeni katika Uwanja wa Shule ya Msingi Orkesumet, ambapo alisema Serikali imedhamiria kuboresha miundombinu ya barabara nchini pamoja na wilaya ya Simanjiro ambapo barabara ya kutoka Kongwa hadi Orkesumet, Simanjiro itajengwa kwa kiwango cha lami.

Alisema barabara hiyo yenye urefu wa km 340 kutoka Kongwa-Mbuyuni NARCO Juntion-Kibaya hadi Orkesumet ipo kwenye ilani ya uchaguzi ya CCM ya 2020-2025. Kukamilika kwa barabara hiyo kutaboresha uchumi wa Simanjiro.

“Barabara nyingine ni Arusha-Kibaya hadi Kongwa (km.430), Kongwa Ranch-Kiteto-Simanjiro hadi KIA (km. 483), Babati-Orkesumet-Kibaya (km. 225). Miradi hii ikikamilika itamaliza changamoto ya miundombinu ya barabara Simanjiro.”


 (mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post