MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amesema sh. bilioni 25.3 zimetumika kuboresha barabara na mitaa ya Manispaa ya Musoma ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya chama hicho ya mwaka 2015 -2020.
“Shilingi bilioni 18.7 zimetumika kujenga km. 14 za barabara kwa kiwango cha lami na kuweka taa za barabarani kupitia Programu ya Uboreshaji wa Miji (ULGSP) katika Manispaa ya Musoma na mradi umekamilika. Tunataka taa ziwake ili usiku uwe mchana, na mchana uwe mchana.”
Alitoa kauli hiyo jana jioni (Jumatatu, Septemba 21, 2020) wakati akizungumza na wakazi wa mji wa Musoma katika mkutano uliofanyika kwenye viwanja vya shule ya Mara Sekondari, katika kata ya Nyamatare, wilayani Musoma, mkoani Mara.
Alisema kupitia Road Fund (Maintenance) kiasi kingine cha sh. bilioni 6.6 kilitumika kwa ajili ya kufungua barabara mpya, kufanya matengenezo ya kawaida na matengenezo ya sehemu korofi na kwamba miradi yote imekamilika.
Mheshimiwa Majaliwa ambaye yuko mkoani Mara kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli alitumia fursa hiyo kuwaombea kura mgombea ubunge wa jimbo la Musoma Mjini, Bw. Vedasto Manyinyi, mgombea udiwani wa kata ya Nyamatare, Bw. Masumbuko Magesa na madiwani wengine wa manispaa hiyo.
“Ninawasihi wana Musoma msisite kumpigia kura Dkt. John Pombe Magufuli hata kama wewe ni mpenzi wa chama kingine kwa sababu yeye ndiye mleta maendeleo kwa nchi yetu,” alisema.
Akielezea mambo mengine yaliyotekelezwa chini ya Ilani hiyo, Mheshimiwa Majaliwa alisema “kampeni ya kumtua mama ndoo kichwani” ililenga kumpunguzia mama kazi ya kutembea umbali mrefu kutafuta maji na badala yake atembee hatua chache kutoka bombani hadi nyumbani akiwa ameshika ndoo yake mkononi.
“Ili kuboresha huduma za upatikanaji wa maji kwenye mji wa Musoma, shilingi bilioni 46 zilitolewa kwa ajili ya mradi mkubwa wa maji safi katika Manispaa ya Musoma ambao tayari umeanza kutoa huduma.”
Alisema sh. bilioni 18 zimetolewa kwa mradi wa kusambaza maji katika Manispaa ya Musoma na vijiji vitatu vya Musoma Vijijini na Butiama, ambapo kazi zinazofanywa ni ujenzi wa tenki la Bharima lenye ujazo wa lita milioni tatu; ujenzi wa kituo cha kusukuma maji (Booster station) na ulazaji wa bomba la kusafirisha maji kwenda kwenye tenki la Bharima (Rising main) lenye kipenyo cha milimita 450 na urefu wa kilomita 1.56.
Alizitaja kazi nyingine zilizofanyika kuwa ni ulazaji wa bomba la kusafirisha maji kutoka kwenye tenki la Bharima kwenda kwa wananchi (Transmission main) lenye kipenyo cha milimita 450 na urefu wa kilomita 7.058; ufungaji wa pampu tatu zenye uwezo wa kusukuma mita za ujazo 175 kwa saa; ununuzi ya bomba za kusambaza maji kilomita 44.3 na ununuzi wa vifaa vya kutendea kazi.
Katika hatua nyingine, Waziri Mstaafu wa Serikali ya awamu ya nne, Mzee Stephen Wassira aliwataka wakazi wa Manispaa ya Musoma wakawapigie kura wagombea kutoka vyama vyenye ilani ya uchaguzi makini kama CCM.
“Tukisema mkapige kura, nendeni mkapige kura kwa wagombea na vyama vyenye Ilani ya Uchaguzi. Si kukupigia chama ili mradi ni safari tu ya kwenda kupiga kura. CCM inazo sera zake na ndiyo maana tunawaomba muwapigie kura wagombea wa CCM,” alisema.
“Hatuwezi kumpa mtu kura za urais kwa sababu tu tumekutana njiani. Rais ni Mkuu wa nchi, Mkuu wa Serikali na Mkuu wa Majeshi. Tunamuombea kura Rais Magufuli kwa sababu amejaribiwa na ameweza.”
Akitoa mfano wa kazi kubwa iliyofanywa na Rais Magufuli mkoani Mara, Mzee Wassira alisema ameweza kukamilisha ujenzi wa hospitali ya Kwangwa ndani ya miaka miaka mitatu, ujenzi ambao ulisimama kwa zaidi ya miaka 40.
Uamuzi wa kujenga ile hospitali ulianzishwa kwa azimio la TANU la mwaka 1974 na likathibitishwa na mkutano mkuu wa TANU mwaka 1974. Hapakuwa na bajeti ya ujenzi, lilikuwa ni suala la kujitegemea. Kwa hiyo, tulianza na michango ya soda ndiyo maana ujenzi wake, umechukua muda mrefu kukamilika,” alisema.