MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka wanaTanga na Watanzania kwa ujumla wahakikishe ifikapo Oktoba 28, mwaka huu wanajitokeza kwa wingi kwenda kumchagua kiongozi mwenye uwezo wa kulinda tunu mbalimbali za Taifa ikiwemo amani na Muungano.
Ameyasema hayo leo (Jumamosi, Septemba 12, 2020) alipokuwa akimuombea kura Rais Dkt. John Pombe Magufuli, mgombea ubunge wa jimbo la Tanga Mjini, Ummy Mwalimu na wagombea udiwani kwa tiketi ya CCM kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika katika viwanja vya Tangamano jijini Tanga.
“WanaTanga bila ya kujali itikadi za vyama nipo hapa mbele yenu kwa unyenyekevu mkubwa nawaomba ifikapo Oktoba 28 mwaka huu tumchague Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli ili akaendeleze miradi ya maendeleo aliyoianzisha. Pia nawaomba tumchague Ummy Mwalimu katika nafasi ya ubunge katika jiji letu la Tanga pamoja na wagombea wa udiwani wa CCM”
Amesema wananchi wanatakiwa wamchague Rais Dkt. Magufuli kwa sababu ni kiongozi shupavu mwenye uwezo wa kufanya maamuzi na asiyekubali kuyumbishwa na yeyote. Pia Rais Dkt. Magufuli ni kiongozi mwenye kuwajali Watanzania na atakayewaruhusu waendelee kuabudu kwa uhuru na ndio maana hata uchaguzi umepangwa kufanyika siku ya Jumatano ili kutoa fursa kwa wananchi kutumia siku za Ijumaa, Jumamosi na Jumapili kwa ajili ya kuendelea kuabudu.
Akizungumzia kuhusu miradi ya miundombinu ya barabara inayotekelezwa katika jiji hilo, Mheshimiwa Majaliwa amesema shilingi bilioni 66.8 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya kutoka Tanga hadi Pangani yenye urefu wa kilometa 50, ambayo inajengwa kwa kiwango cha Lami.
“Shilingi bilioni 2.3 zimetumika kwa ajili ya uwekaji wa taa za barabarani 436 kwa barabara zilizopo ndani ya Jiji la Tanga na taa za kuongoza magari katika barabara ya Mombasa. Ujenzi wa miundombinu hii umeinua uchumi wa wananchi wa Jiji la Tanga kwa kuwawezesha kufanya kazi zao bila vikwazo.”
Amesema miradi mingine ya kimkakati inayotekelezwa katika jiji hilo ni pamoja na ujenzi wa dampo la kisasa katika eneo la Mpirani Chongoleani ambapo shilingi bilioni 8.9 zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa eneo la udhibiti wa taka ngumu na tayari ujenzi umekamilika.
Mheshimiwa Majaliwa amesema jumla ya shilingi bilioni 1.7 zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa kitega uchumi kwenye stendi ya mabasi ya Jiji la Tanga. Ujenzi unaendelea na upo katika hatua ya umwagaji zege katika ghorofa ya pili.
“Shilingi bilioni 21.9 zimetumika kuboresha miundombinu ya barabara zenye urefu wa kilometa 16.4 kwa kiwango cha lami. Barabara hizo zilizotengenezwa ni barabara ya Sita na barabara ya Chumbageni (km 1), Barabara ya Nne na Chumbageni hadi Ikulu (km 1.14), Barabara ya kutoka Diwani/Ikulu, Taifa na Sahare Phase. I (km 4.2).”
Amesema barabara nyingine ni barabara ya kutoka Diwani hadi Mwabonde (km 1.62), barabara ya kutoka Mabawa - Msambweni II (km 0.80), barabara ya kutoka Mabawa, barabara ya Nguvumali, barabara ya Nane na Jamatcan (km 3.53), Barabara ya Msambweni na Barabara ya stendi ya Kange (km 5.0).
Mheshimiwa Majaliwa amesema shilingi bilioni 2.2 zimetumika kwa ajili ya ujenzi wa mifereji mikubwa ya maji ya mvua yenye urefu wa kilometa 3.44 jijini Tanga. Pia shilingi bilioni 10 zimetumika kuboresha miundombinu ya barabara kwa kiwango cha changarawe na udongo katika maeneo mbalimbali ya Halmashauri ya Jiji la Tanga.
Amesema katika mwaka wa fedha wa 2020/2021 Halmashauri ya jiji la Tanga imepanga kutumia shilingi bilioni 1.3 kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Mabawa- Msambweni II na barabara ya 11 na ya 12 kwa kiwango cha lami, ambapo kwa sasa utekelezaji wake upo katika hatua za awali
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,