MAJALIWA: ILANI YA CCM YAFANIKISHA MASOKO 28 YA MADINI KUANZISHWA

SERIKALI ya Chama cha Mapinduzi imeanzisha masoko 28 ya madini likiwemo la Nyamongo ili kuwainua wachimbaji wadogo ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya 2015-2020.

Hayo yamebainishwa jana (Jumapili, Septemba 20, 2020) na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa alipokuwa akizungumza na wakazi wa Nyamongo, Nyamwaga na Tarime Mjini, wilayani Tarime, mkoani Mara alipokuwa akimuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli na wagombea ubunge wa jimbo la Tarime Mjini, Bw. Michael Kembaki, na Tarime Vijijini, Bw. Mwita Waitara na wagombea udiwani wa kata zote za wilaya ya Tarime.


“Kupitia mradi wa usimamizi endelevu wa rasilimali za madini, Serikali imeanzisha masoko 28 ya madini, vituo vidogo 28 vya ununuzi wa madini na ujenzi wa vituo saba vya mafunzo ya umahiri kwa wachimbaji wadogo vya Bariadi, Musoma, Bukoba, Mpanda, Chunya, Songea na Handeni,” amesema.

“Hatua hizi pamoja na kusaidia kuongezeka kwa mapato ya Serikali zimesaidia kupata takwimu sahihi za mauzo ya madini, kuwasaidia wachimbaji wadogo kupata soko la uhakika, kupata bei stahiki kwa bidhaa za madini, kuondoa tatizo la utoroshaji na biashara haramu ya madini,” amesema.

Akiwafafanulia mambo yaliyofanywa na Serikali ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya CCM ndani ya miaka mitano, Mheshimiwa Majaliwa amesema baadhi ya kodi kwenye biashara ya madini zenye kero kwa wachimbaji wadogo ikiwemo kodi ya zuio (withholding tax) asilimia tano na kodi ya ongezeko la thamani (VAT) asilimia 18 zimeondolewa.

Akielezea tathmini ya fidia kwa wananchi wa Nyamongo, Mheshimiwa Majaliwa amesema uthamini kwa ajili ya ujenzi wa bwawa la maji machafu eneo la Nyamongo kwa vijiji vya Matongo, Nyabichune na Komarera ulianza Julai, 2019 na malipo ya fidia yalianza kutolewa Mei 2020.

“Hadi sasa shilingi bilioni 32.9 zimelipwa kwa wananchi 1,620 na wananchi 13 wamebaki ambao hawajachukua malipo yao yenye thamani ya shilingi milioni 833. Hao 13 wanasubiri kulipwa kwa sababu walisema hawaridhiki na uthamini wa mali zao, kwa hiyo tathmini itafanyika upya na watalipwa fedha zao,” amesema.

Kuhusu maji safi na salama, Mheshimiwa Majaliwa amesema sh. bilioni 1.1 zimetolewa kwa ajili ya uboreshaji wa miradi ya maji ambapo sh. milioni 50.3 zilitumika kwa ujenzi wa mradi wa maji Gamasara na umekamilika.

“Fedha nyingine, shilingi bilioni 2 zilitumika kwa ukarabati wa skimu ya maji Nyamwaga na imekamilika; shilingi milioni 11.2 zilitumika kwa ukarabati wa skimu ya maji Korotame ambayo nayo imekamilika; shilingi milioni 35 zilitumika kwa ukabati mradi wa maji Nyarwana na umekamilika,” amesema.

Amesema sh. milioni 247 zilitumika kwa ukabati mradi wa maji vijiji ya Keisangora na Nyamwaga na ukarabati unaoendelea huku sh. milioni 90 zikiwa zimetumika kwa ukarabati mradi wa maji Gibaso ambako pia ukarabati bado unaendelea. Pia sh. milioni 300 zilitumika kwa ukabati mradi wa maji Borega “A” na ukarabati unaendelea.

Amesema jumla ya shilingi milioni 137.6 zimetumika kwa ukarabati wa pampu za mkono 46 na uchimbaji wa visima vitano katika vijiji vya Kwisarara, Borega A, Nyantira, Kitawasi na Gibaso.

Kuhusu umeme, Mheshimiwa Majaliwa vijiji 62 kati ya vijiji 88 vya Halmashauri ya Wilaya ya Tarime vimepata umeme. Vijiji vilivyobakia ni 26.

Ameviataja vijiji ambayo umeme haujafika ni Korotambe, Nyakangara, Keroti, Kiongera, Kikomori, Nyabirongo, Nyabichune, Pemba, Kyoruba, Nyabitocho, Kitenga, Kitawasi, Masurura, Kenyamosabi, Msege, Gibaso, Karakatonga, Nyabirongo, Kegonga, Nyandage, Nyamombara, Nyankoni, Soroneta, Magoma, Nyasaricho na Kebweye.

(mwisho)
   
IMETOLEWA:
JUMAPILI, SEPTEMBA 20, 2020.




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post