Ametoa kauli hiyo leo (Jumatatu, Septemba 21, 2020) wakati akizungumza na wakazi wa Kata ya Bukima, wilayani Musoma, mkoani Mara katika mkutano uliofanyika kwenye viwanja vya shule ya msingi Majita.
Mheshimiwa Majaliwa ambaye yuko mkoani Mara kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli alitumia fursa hiyo kuwaombea kura mgombea ubunge wa jimbo la Musoma Vijijini, Prof. Sospeter Muhongo na madiwani wengine wa wilaya hiyo. Mgombea udiwani wa kata ya Bukima, Bw. Januari Simla alipita bila kupingwa.
“Katika kutekeleza Ilani ya CCM, tumepunguza kodi kwenye malighafi na zana za uvuvi, kwenye injini za uvuvi, nyuzi za kushonea nyavu za kuvulia samaki, vifungashio na kwenye ada za leseni za kuvulia samaki,” amesema.
Akielezea mambo mengine yaliyofanyika kwenye sekta hiyo, amesema kazi kubwa iliyofanyika ni kuwatambua wavuvi na kuwaweka kwenye vikundi kazi ambayo alisema imesaidia kuongeza vikundi hivyo kutoka 37 hadi kufikia 113.
“Ni kwa nini tuliamua kuwaweka kwenye vikundi, ni kwa sababu inakuwa rahisi kuwafikia, kuwaelimisha na kuwahudumia. Hii imefanikisha idadi ya samaki wanaovuliwa iongozeke kutoka samaki 415,000 hadi kufikia zaidi ya 800,000.”
Amesema kiwango cha uvuaji samaki kimeongezeka kutoka tani 300 na kufikia tani 448, 467. “Kikubwa ninachowaomba ni kwamba, tumieni vyombo vya kisasa kuvua samaki ili kutunza mazalio yao.”
Akiwa njiani kuelekea Musoma Mjini, Mheshimiwa Majaliwa alisimamishwa na wakazi wa kata za Kusenyi, aliwasalimia wakazi wa kata za Mugango na Mkirira, ambako pia aliwaombea kura wagombea wa urais, ubunge na udiwani kwa tiketi ya CCM.