Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MAJALIWA: SERIKALI INAWATHAMINI WAFUGAJI NCHINI


MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali inawathamini wafugaji na itaendelea kuboresha sekta yao.

Ameyasema hayo leo (Jumatano, Septemba 16, 2020) wakati akiwasalimia wananchi waliojitokeza kumlaki kwenye kata ya Bukundi, tarafa ya Nyaranje, wilayani Meatu akiwa njiani kutokea Mkalama, Singida.

"Tunatambua na kuwathamini sana wafugaji kwa sababu tunajua mifugo ni fedha," amesema wakati akimuombea kura mgombea Urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli, mgombea ubunge wa jimbo la Meatu, Bi. Leah Komanya na Mgombea udiwani wa kata ya Bukundi, James Sombi.

"Serikali yenu imedhamiria kuboresha sekta ya mifugo nchi nzima na ndiyo maana Waziri mwenye dhamana ya mifugo amekuwa anakutana na wafugaji nchi nzima ili waeleze ni maeneo gani yanawapa kero."

Amesema Serikali iliruhusu vijiji 920 kati ya 970 vilivyokuwa kwenye maeneo ya hifadhi virasimishwe ili wananchi waendelee na ufugaji na kilimo.

Amesema eneo la Bukundi lina wakazi wengi ambao asilimia 60 kati ya hao ni wafugaji. Kwa hiyo amewaomba wagombea hao wakipita, warudi kwa wananchi na kutatua kero zao kwenye sekta ya mifugo.

Mapema, mgombea ubunge wa jimbo la Kisesa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Bw. Luhaga Mpina alisema wakati Serikali ya awamu ya tano inaingia madarakani, majosho 1,000 kati ya 2,400 yaliyokuwepo yalikuwa ni mabovu.

"Chini ya uongozi wa Rais wetu jemedari, Dkt. Magufuli, majosho 600 yamekarabatiwa na tumejenga majosho mengine mapya 104. Yote yamepewa dawa ya ruzuku na wafugaji wanayatumia kuosha mifugo yao," alisema.

(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com