MAMBO YATAKAYOFANYWA NA CHADEMA SIKU 100 ZA KWANZA IKISHINDA URAIS


Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimeainisha mambo 16 kitakachofanya siku 100 za kwanza iwapo kitachaguliwa na kupewa ridhaa ya kushika dola katika uchaguzi wa rais, wabunge na madiwani utakaofanyika Oktoba 28, mwaka huu.

Katika Ilani yake yenye kurasa 104, chama hicho kimetaja mambo 16 ya kipaumbele ambayo yatatekelezwa siku 100 za kwanza, ambayo pamoja na mambo mengine itapeleka bungeni muswada wa sheria mbalimbali ikiwamo ya maridhiano.

Pia, ilani hiyo imeainisha vipaumbele 20 katika kujenga nchi yenye demokrasia, utawala bora na haki za binadamu.

Ilani hiyo imebainisha kuwa serikali ya CHADEMA itapeleka bungeni muswada wa sheria ya maridhiano ambayo pamoja na mambo mengine, itaanzisha Tume ya Maridhiano kwa lengo la kuondoa hofu ya uwezekano wa vitendo vya kulipiza visasi na kuunganisha nguvu za wananchi wote bila ubaguzi wa vyama katika kuongoza taifa.

Pia imejinasibu kuwa ndani ya siku hizo itapeleka bungeni muswada wa marekebisho ya Sheria ya Hifadhi ya Jamii ili kurekebisha kikokotoo cha Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwa wastaafu ili kiendane na mahitaji ya wastaafu.

“Serikali ya CHADEMA itaruhusu wafanyakazi na watumishi waliochangia katika mifuko ya jamii kuchukua mafao yao wakati wowote (Fao la kujitoa),” ilisema.

Ilani hiyo imebainisha kuwa itapeleka muswada wa sheria ya ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi juu ya utoaji wa elimu bure kuanzia elimu ya awali hadi sekondari.

Aidha, imesema itapunguza kiwango cha marejesho ya mikopo ya elimu ya juu hadi kufikia asilimia tatu ya mshahara wa mnufaika na kutanua wigo wa muda wa marejesho hadi kufikia miaka 25 tangu mnufaika apate ajira.

Kadhalika, imesema itafuta riba na tozo zote zitokanazo na adhabu ya kuchelewesha marejesho ya mkopo wa elimu ya juu.

“Serikali ya CHADEMA itashirikiana na sekta binafsi kuweka utaratibu wa kutoa huduma za afya ya msingi kwa wananchi bila malipo,” ilisema sehemu ya ilani hiyo.

Kwa mujibu wa ilani hiyo, serikali hiyo itarejesha mchakato wa Katiba Mpya kuanzia iliyoishia Rasimu ya Tume ya Marekebisho ya Katiba ya Jaji Warioba.

Aidha, Serikali ya CHADEMA itatekeleza matakwa ya Katiba kuhusu Tume ya Pamoja ya Fedha ya Muungano ili kila nchi mshirika wa Muungano ipate mgawo wake wa fedha kwa mujibu wa Katiba na sheria.

Pia CHADEMA imejinasibu kuwa itarejesha uhuru wa vyombo vya habari ikiwa ni pamoja na kuruhusu kurushwa moja kwa moja vikao vya kamati za Bunge, mikutano ya Bunge na mwenendo wa uendeshaji wa mashauri mahakamani.

Kwa mujibu wa Ilani hiyo, CHADEMA imesema itaanzisha utaratibu wa mazungumzo kati ya serikali ya Jamuhuri na Zanzibar kwa lengo la kufikia muafaka juu ya utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi, uvuvi wa bahari kuu na usajili wa meli.

“Serikali ya CHADEMA itaandaa mazingira rafiki na wezeshi kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari walioshindwa kuendelea na masomo kwa sababu mbalimbali kama vile ugonjwa, kukosa ada, mimba kurejea kwenye mfumo rasmi wa elimu na kuamlizia masomo yao,” ilisema sehemu ya ilani hiyo.

Aidha, ilani hiyo ilibainisha kuwa itapeleka bajeti ya nyongeza bungeni katika mwaka wa fedha 2020/21 kwa ajili ya kuongeza mishahara ya watumishi wote wa umma, kulipa malimbikizo, sambamba na kuwapandisha madaraja watumishi wenye sifa na kulipa mishahara inayoendana na madaraja yao.

Pia imesema itaanzisha bima maalum ya afya kwa watumishi wote wa vyombo vya ulinzi na usalama wawapo kazini na baada ya kustaafu vikiwamo Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Polisi, Magereza, Uhamiaji, Zimamoto na Uokoaji.

CHADEMA imesema itarejesha maduka yasiyotozwa kodi katika vyombo vya ulinzi na usalama vikiwamo Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Polisi, Magereza, Uhamiaji, Zimamoto na Uokoaji.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post