Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MBINU ZA USTAWI WA KILIMO CHA MKONGE KANDA YA ZIWA ZATOLEWA

Samirah yusuph
Simiyu.Bodi ya Mkonge Tanzania imekabidhi kitabu cha muongozo wa kilimo cha mkonge kwa wadau wa kilimo mkoa wa hapa, ili kuhakikisha mkulima anazalisha mkonge ulio na ubora na kuuza kwa thamani zaidi sokoni.

Akikabidhi muongozo huo mratibu mkuu wa utafiti na masoko Hassan Kibarua alisema kuwa, mkonge wa kanda ya ziwa ni mrefu zaidi hivyo inatakiwa wakulima waelimishwe namna ya kuuchakata kwa utaalam ili usipungue thamani.

"Mkonge unatakiwa kuchakatwa si zaidi ya masaa 48 tangu umekatwa lakini unakuta mkulima anachakata mkonge uliokatwa zaidi ya siku tano, unakuwa umepungua ubora na unapofika sokoni unakuwa haupo kwenye daraja la ubora wa 3L ambalo lina bei ya juu," alisema Kibarua.

Aliongeza kuwa pia wakulima inabidi waelekezwe namna ya kuchakata na kusafisha mkonge ili wasipeleke sokoni mkonge wenye uchafu (maganda) kwani makosa kidogo yanapelekea kushuka kwa thamani ya zao hilo.

Awali akifafanua umuhimu wa kupima afya ya udongo ili kuongeza uzalishaji wa mkonge, mratibu wa utafiti wa udongoTanzania kutoka TARI- Mlingano Dr Sibaway Mwango, alisema kuwa maafisa ugani wawe ni daraja la kuwaunganisha watafiti na wakulima.

"Afya ya udongo ni muhimu zaidi kwa kilimo chenye tija hivyo afisa ugani anajukumu la kuhakikisha kuwa mkulima anahamasika kufanya vipimo hivyo," alisema Dr Mwango.

Alisema, lengo ni kulinda afya ya udongo na kuepuka matumizi ya mbolea yasiyo sahihi yanayo sababisha kuharibu udongo na mkulima anashindwa kupata mavuno stahiki kulingana na ukubwa wa ardhi.

Katika mkoa wa Simiyu zao la mkonge tayari limeanza kulimwa na wakulima katika baadhi ya maeneo hasa katika wilaya ya Meatu na Maswa ambao hupeleka mkonge wao katika shirikisho la wakulima wa mkonge Kishapu (SHIWAMKI) mkoani Shinyanga.

Baadhi ya wakulima hao wameeleza namna ambavyo wanaendesha kilimo hicho na kuwa hapo awali hawakujua kuwa mkonge ni mali hadi walipo pata elimu ya kilimo hicho na kukifanyia kazi na sasa wananufaika nacho.

"Uzuri ni kwamba mkonge haubagui ukame wala mvua nyingi kwa hali yoyote ni lazima uvune na ninachanyanya na mazao yangu mengine ya msimu mfano mahindi na pamba" alisema Mabula Kipawa mkulima wa mkonge wilayani Meatu.

"Ukiangalia uchumi wangu wa sasa na hapo awali kunamabadiliko sana sasa ninalima kilimo ambacho kinaniingizia pesa muda wowote hadi nimefikia hatua ya kuweza kupeleka watoto wangu shule na kuwa na uchumi mzuri,"alisema Mizwazwa Kidia mkulima wa mkonge kata ya Mwasengea.

Licha ya kuwa wamekuwa wakipata faida katika kilimo hicho wakulima hao wameibainisha kuwa usafiri ni changamoto ambayo inawakwamisha wakulima wengi kulima zao hilo.

"Usafiri ni shida kwa sababu unasafirisha mzigo kutoa shambani ukimaliza kuchakata unasafirisha kwenda kishapu kwenye shirikisho, kisha unasafirishwa tena kwenda Tanga ndipo uende sokoni, unajikuta unabaki na faida ambayo pengine usafiri ungekuwa rahisi ingekuwa kubwa mara dufu," aliongeza Mizwazwa.

Mwisho.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com