Mgombea Ubunge Viti Maalumu Mkoa wa Dodoma kupitia CCM, Halima Okash, akipiga magoti kumuombea kura Mgombea Urais wa Tanzania kupitia CCM, wakati wa kampeni zilizofanyika Kata ya Nala, jijini Dodoma.
Na Richard Mwaikenda, Dodoma
MGOMBEA Ubunge Viti Maalumu Mkoa wa Dodoma kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Halima Okashi (pichani) amewastajabisha watu alipoamua kupiga magoti kumuombea kura Mgombea Urais wa Tanzania kupitia CCM, Dk. John Magufuli wakati wa kampeni za chama hicho katika Kata ya Nala Jimbo la Dodoma Mjini.
Okashi alisema kuwa ameamua kufanya hivyo hasa kutokana na kwamba wananchi wa Dodoma hawana cha kumlipa Rais Magufuli kwa mambo mengi mazuri aliyoyafanya isipokuwa zawadi pekee ya kumpa ni kumpigia kura nyingi katika Uchaguzi Mkuu Oktoba 28, mwaka huu.
Mgombea huyo kupitia Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) aliwaomba wanawake, vijana na wazee siku hiyo kujitokeza kwa wingi kumpigia kura Dk. Magufuli, wabunge na madiwani wa CCM.
Amewataka wanawake popote walipo nchini kulinda kura katika familia zao bila kuchoka hadi siku ya kupiga kura na kuhakikisha zote zinakwenda kwa wagombea wa CCM.
Pia, Okashi amesema haoni sababu ya Dk. Magufuli kutompa miaka mingine mitano, kwani ameonesha dhahiri kwa muda mfupi wa miaka mitano iliyopita kwa jinsi alivyoifanyia nchi mambo mengi makubwa ambayo kila mwenye macho haambiwi tazama.
Okash akielezea mambo mbalimbali mazuri yaliyofanywa na Rais Magufuli kwa kipindi cha miaka mitano ikiwemo kuhamishia makao makuu ya nchi mkoani Dodoma kitendo ambacho kimeupa hadhi kubwa mkoa huo.
Social Plugin