Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

OPERESHENI ZA TAKUKURU MKOANI SINGIDA ZAOKOA SHILINGI 199,559,254/= IKIWEMO MIKOPO UMIZA

Na Mary Mwakapenda, Manyoni
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Singida imefanikiwa kuokoa kiasi cha Tsh. 199,559,254/= kufuatia operesheni mbalimbali zilizofanywa ili kuzuia na kupambana na vitendo vya rushwa mkoani humo katika kipindi cha kuanzia Julai 2019 hadi Juni 2020.

Hayo yamesemwa jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt (Mst) Mhe. George H. Mkuchika wakati akimkaribisha Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Job Ndugai kuzindua jengo la Ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Manyoni mkoani Singida.

 Mkuchika ameyataja baadhi ya maeneo ambayo operesheni hiyo iliyalenga kuwa ni pamoja na mikopo umiza ambapo kiasi cha Tsh. 58,150,000/= kiliokolewa, kwa upande wa mapato yatokanayo na usimamizi wa madini, kiasi cha Tsh. 44,623,254/= kiliokolewa, sanjari na hayo, kiliokolewa kiasi cha Tsh. 11,456,500/= kutokana na mapato ya usimamizi wa minada, na kiasi cha Tsh. 85,329,500/= kilirudishwa kutoka kwa wanachama wa vyama vya ushirika.

 Mkuchika amefafanua kuwa, jitihahada zote hizi zilizofanywa na zinazoendelea kufanywa na TAKUKURU zinatokana na weledi, ujasiri na uzalendo uliopo katika kushughulikia tatizo la rushwa nchini, hivyo ameitaka TAKUKURU kuendelea na kasi hiyo ili kudhibiti vitendo vya rushwa na ufisadi nchini.

Katika eneo la utoaji elimu dhidi ya vitendo vya rushwa, Mhe. Mkuchika ameanisha kuwa, TAKUKURU imefanikiwa kufungua na kuimarisha klabu 234 za Wapinga Rushwa mashuleni na vyuoni na kutoa semina pamoja na mikutano ya hadhara 225.

Aidha, Mhe. Mkuchika amemuahidi Mhe. Ndugai kujenga Ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Kongwa ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli alilolitoa tarehe 22 Julai, 2020 wakati akifungua jengo la Ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Chamwino na kuongeza kuwa, hatua hii inadhirisha nia ya dhati ya Serikali ya kupambana na vitendo vya rushwa nchini.

Jengo la Ofisi ya TAKUKURU la Wilaya ya Manyoni ni mojawapo ya majengo saba ambayo Mhe. Rais Magufuli alitakiwa kuyafungua kwa pamoja tarehe 22 Julai, 2020 wakati akifungua jengo la Ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Chamwino, Dodoma. Hata hivyo, aliweka utaratibu wa kuyafungua kwa nyakati tofauti na kumuelekeza Mhe. Ndugai kulifungua jengo hilo.
 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt (Mst) George Mkuchika akitoa maelezo kuhusu jengo la TAKUKURU Wilaya ya Manyoni kabla ya kumkaribisha Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Job Ndugai kuzungumza na wananchi na kulizindua jengo hilo.
 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt (Mst) George Mkuchika akimkaribisha Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Job Ndugai kuzungumza na wananchi kabla ya kuzindua jengo la Ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Manyoni mkoani Singida jana.
 Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Job Ndugai akizungumza na wananchi wilayani Manyoni jana kabla ya kuzindua jengo la Ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Manyoni mkoani Singida.
 Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Job Ndugai (kushoto) akisoma kibao cha ufunguzi wa jengo baada ya kuzindua jengo la Ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Manyoni mkoani Singida jana. Wanaoshuhudia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt (Mst) George Mkuchika na Mkuu wa Wilaya ya Manyoni, Bibi Rahabu Magwisa.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt (Mst) George Mkuchika akiipongeza Klabu ya Wapinga Rushwa ya Shule ya Sekondari ya Mlewa Wilayani Manyoni wakati wakiimba wimbo wa mapambano dhidi ya rushwa kwenye hafla ya uzinduzi wa jengo la Ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Manyoni mkoani Singida jana.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com