Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

POLEPOLE: HATA WAKIUNGANA, TUTAWASHINDA KWA KISHINDO



 Chama cha Mapinduzi kimesema kuwa kinasubiria kwa hamu ushirikiano wa baadhi ya vyama vya upinzani, kwani kushirikiana kwao hakutazuia CCM kuibuka washindi katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 28, 2020.




Akitoa tathmini ya mwenendo wa kampeni za chama hicho, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole amesema chama hicho kimeendelea na kampeni za kistaarabu na kitapata ushindi wa kishindo mwaka huu.

Kauli yake imekuja siku chache baada ya CHADEMA na ACT Wazalendo kuonesha nia ya kutaka kushirikiana katika ngazi ya Urais, jambo ambalo limepokelewa kwa mitazamo tofauti na wananchi.



“Mimi natoa rai wasisubiri Oktoba 3 ili waungane, hawa waungane sasa halafu ndiyo watajua tulipotoka na tulipofika na Watanzania, sisi tumeingia nchi hii ni maskini huyu mzee Magufuli kapambana leo sisi ni nchi ya uchumi wa kati

“Yule mgombea wa chama cha bwana Zitto kule Zanzibar tutamshinda katika namna ambayo watu wake wa karibu wakae naye karibu, kwa sababu ushindi wa kipindi hiki utakuwa ni mkubwa mno kiasi kwamba wakae karibu  kumtia moyo"-Polepole

Mbali na hilo amewataka Watanzania kupuuza baadhi ya hoja ambazo amesema si za ukweli zinazoenezwa na wagombea wa upinzani ikiwemo madai kuwa Kampuni ya Ndege ya Tanzania (ATCL) haikukaguliwa matumizi yake, ununuzi wa ndege ulikuwa nje ya bajeti na kwamba viwanja vya ndege vinajengwa kwa kuangalia maeneo walimotoka viongozi.

Akitolea mfano Uwanja wa Ndege wa Mpanda, Polepole amesema “… haukujengwa kwa sababu ya Mizengo Kayanza Peter Pinda. Wengi wanaotumia uwanja huo ni watalii wanaokwenda Mbuga ya Wanyama ya Katavi.”


Kuhusu madai kuwa Dkt. Magufuli anatumia mamlaka ya Urais kwenye kampeni, Polepole amesema kuwa licha ya kuwa kampeni zinaendelea lakini serikali bado ipo kazini na kwamba Rais anakoma kushika wadhifa huo pale mwingine anapoapishwa.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com