Mwinjilisti wa Kimataifa kutoka Huduma ya New Life Outreach ya jijini Arusha, Dkt. Egon Falk, akihubiri katika mkutano mkubwa wa injili uliofanyika jana katika Viwanja vya Shule ya Msingi Ukombozi mjini Singida. Mkutano huo ambao utafanyika kwa siku tano umeandaliwa na Umoja wa Makanisa ya Kipentekosti (FPCT) mkoani hapa kwa kushirikiana na Huduma ya New Life Outreach ya jijini Arusha.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi, akizungumza wakati akifungua mkutano huo.
Mwinjilisti wa Kimataifa Dkt. Egon Falk, akiwa na mke wake kwenye mkutano huo.
Hamasa ya kusifu ikitolewa kwenye mkutano huo.
Mwenyekiti wa Umoja wa Makanisa ya Kipentekosti (CPCT) Manispaa ya Singida, Mchungaji Boniface Ntandu akizungumza kwenye mkutano huo.
Mwinjilisti wa Kimataifa Dkt. Egon Falk, akimkabidhi Printa, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi kwa ajili ya Shule ya Msingi Ukombozi.
Kiongozi wa mkutano huo, Mchungaji Peter Kokonyo, akizungumza.
Mkutano ukiendelea. Kushoto ni Askofu Amos Magasi, Mkuu wa Makanisa ya FPCT Mkoa wa Singida.
Mkutano ukiendelea.
Maombi yakiendelea kufanyika. Katikati (mwenye suti nyeusi) ni Mratibu wa Huduma ya New Life Outreach, Japhet Barashikwa.
Kiongozi wa kundi la nyimbo za sifa, Eliudi Zabroni akiwajibika jukwaani.
Viongozi wakiwa jukwaa kuu.
Wahudumu wakitoa msaada kwa watu waliofanyiwa maombi kwenye mkutano huo.
Na Mwandishi Wetu, Singida.
MKUU wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi amewakumbusha wananchi kutambua kuwa Mungu yupo kwani amewaepusha na majanga mengi ikiwemo ugonjwa wa Corona.
Dkt. Nchimbi aliyasema hayo jana alipoalikwa kufungua mkutano wa injili ulioanza jana katika Viwanja vya Shule ya Msingi Ukombozi mjini Singida mkutano ulioandaliwa na Umoja wa Makanisa ya Kipentekosti (FPTC) mkoani hapa kwa kushirikiana na Huduma ya New Life Outreach ya jijini Arusha inayoongozwa na Mwinjilisti wa Kimataifa Dkt. Egon Falk.
Alisema kuwa Rais Magufuli kutokana na kutambua kuwa Mungu yupo alitangaza maombi ya kumuomba Mungu ili kuwaepushia ugonjwa wa Corona kwa watanzania na Mungu alisikia maombi hayo.
"Haiwezekani Mungu huyu aliyetuondolea Corona halafu eti tuendelee kusema Singida ni maskini, Tanzania ni maskini wakati kuna raslimali, haiwezekani." alisema Dkt Nchimbi.
Pia Nchimbi aliwataka wananchi kuwa uchaguzi usiwatenganishe na Mungu badala yake waungane kwa pamoja bila kuangalia madhehebu yao ili kuijenga nyumba ya bwana ambayo ni Mkoa wa Singida na Tanzania kwa ujumla.
"Katika uchaguzi wa mwaka huu tuende tukabariki sio kuchinja,Vitambulisho tulivyonavyo tukavitumie katika kubariki na sio kuchinja kama wanavyosema wengi." alisema.
Kwa upande wake Mwinjilisti wa Kimataifa Dkt. Egon Falk akihubiri katika mkutano huo aliishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuruhusu mikutano ya injili kufanyika hadharani nakuwa amekuwa akifanya kazi hiyo hapa nchini sasa ni takribani miaka 46 pasipo kuzuiliwa.
"Takribani miaka 46 sasa niko hapa Tanzania nikihubiri neno la Mungu,sijawahi kuzuiliwa na kiongozi yeyote, sijawahi kuona kiongozi yeyote wa nchi duniani akitangaza siku tatu za maombi ya kufunga ni Tanzania pekee Mungu awabariki sana watanzania." alisema Egon.
"Ulaya watu wamebarikiwa wamekuwa na maendeleo lakini hawamtambui Mungu, nawaomba watanzania mkipata maendeleo msimsahau Mungu." alisema.
Aidha Dkt. Egon alitoa zawadi ya Printa kwa Shule ya Msingi Ukombozi anapofanyia mkutano huo ambapo alimkabidhi mkuu wa mkoa ambaye alimkabidhi Mwalimu Mkuu Msaidizi wa shule hiyo, Gregory Manimo kwa niaba ya mwalimu mkuu.