Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Serikali Kutokomeza Wadudu Waenezao Magonjwa Ya Mifugo


Na. Edward Kondela
Serikali imelenga kukabiliana na magonjwa ya mifugo nchini kupitia taasisi zilizo chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi, kwa kutumia njia ya chanjo pamoja na kutokomeza wadudu wakiwemo mbung’o ambao wanaathiri afya ya wanyama.

Akizungumza katika ziara ya kikazi ya siku moja aliyofanya Mkoani Tanga mwishoni mwa wiki hii, baada ya kutembelea Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel amewataka watanzania kutambua kazi kubwa zinafonywa na taasisi za serikali katika kufanya tafiti na kutafuta tiba ya magonjwa ya mifugo nchini.

“Wito wangu kwa wafugaji ambao bado wanasumbuliwa na mbung’o, tayari kituo chetu cha TVLA Mkoani Tanga wameshapata njia nzuri na rahisi kabisa, lengo kubwa kabisa ni kuhakikisha tunatokomeza magonjwa ya mifugo kadri inavyowezekana, niombe watanzania watambue kazi kubwa zinazofanywa na taasisi zetu, ili tuondoke katika ufugaji wa mazoea bali sasa tufanye ufugaji wa kisayansi.”  Amesema Prof. Gabriel

Afisa Utafiti wa Mifugo kutoka TVLA Mkoani Tanga Bw. Peter Lucas, amemfahamisha Prof. Gabriel kuhusu njia rahisi ambazo wafugaji wanaweza kutumia katika kutokomeza mbung’o kuwa ni pamoja na mtego wa kukamata mbung’o na njia ya kuweka dawa maalum ya kuua mbung’o kwenye vitambaa vyenye rangi ya bluu na nyeusi ambazo zimekuwa zikiwavutia wadudu hao.

Akiwa katika chuo cha Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA) Kampasi ya Buhuri Mkoani Tanga, Katibu Mkuu Prof. Gabriel amewataka wakufunzi wa chuo hicho wawe na upeo mkubwa ili waweze kutoa wahitimu waliopata elimu bora.

“Kikubwa wafundisheni wanafunzi kujiajiri na anayefundisha somo hilo lazima awe amejiajiri, lazima tuwajengee wanafunzi wetu kazi siyo mpaka kuajiriwa, kujiajiri pia ndiyo msingi hasa wa kuendeleza maendeleo na nchi zilizoendelea walioleta maendeleo ni wajasiriamali.” Amefafanua Prof. Gabriel.

Katika ziara hiyo ya siku moja Mkoani Tanga, Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel alijionea shughuli zinazofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) mkoani humo, ambapo ameitaka taasisi hiyo kutoa taarifa ya tafiti mbalimbali za mifugo ikiwemo ya ng’ombe bora wa maziwa na kuongeza idadi ya mifugo iliyopo katika eneo hilo.

Aidha, akizungumza na watumishi wa taasisi hizo Prof. Gabriel amewataka watumishi hao kuwa wazalendo na kujituma kwa kutoa michango yenye tija katika taasisi wanazofanyia kazi.

Wakizungumza katika nyakati tofauti Kaimu Meneja wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), Dkt. Oliva Manangwa amemuarifu katibu mkuu huyo kuwa TVLA imefanikiwa kufanya tafiti mbalimbali ikiwemo ya kutokomeza kabisa vimelea vya ndorobo visiwani Zanzibar kwa kuwahasi mbung’o dume.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) Mkoa wa Tanga Dkt. Zabron Nziku amemweleza Katibu Mkuu Prof. Gabriel kuwa wameanzisha maabara ya kisasa kwa ajili ya kutengeneza virutubisho vya mifugo vinavyotokana na zao la muhogo ambavyo havina gharama kubwa kwa wafugaji.

Naye Meneja wa Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA) Kampasi ya Buhuri Mkoani Tanga Bw. Venance Tarimo amesema chuo hicho kimekuwa kikitoa mafunzo ya muda mfupi na muda mrefu ili kupata wataalam bora wa mifugo nchini.

Akihitimisha ziara ya kikazi ya siku moja Mkoani Tanga katika taasisi zilizo chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Katibu Mkuu wa wizara hiyo anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel amekutana na Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga Bi. Judica Omari na kuzungumzia changamoto mbalimbali zinazowakumba wafugaji katika mkoa huo na namna ya kuzitatua.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel alikuwa katika ziara ya kikazi ya siku moja Mkoani Tanga mwishoni mwa wiki hii ili kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA) na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) ambazo zote zipo chini ya wizara hiyo.

Mwisho.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com