Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TBS YAFIKIA WADAU ZAIDI YA 3OO WA MAFUTA



Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limeandaa mpango wa mafunzo kwa wazalishaji, wasambazaji na wauzaji wa mafuta ya kula mkoani dodoma yatakayofanyika halmashauri ya wilaya ya Kondoa , Kongwa, Mpwapwa, Kibaigwa na Chamwino, Dodoma jiji, Bahi, Manyoni na Itigi. 


Mafunzo haya yamelenga kuwaelimisha wadau hao juu ya uzalishaji bora, uhifadhi sahihi wa bidhaa za mafuta haswa sehemu za kuuzia, ufungashaji sahihi na salama na umuhimu wa kuzingatia na kuweka taarifa sahihi na muhimu katika vifungashio.

TBS imetoa elimu hii kwa kushirikiana na Wizara ya viwanda, maafisa biashara, afya na maendeleo wa wilaya ili kuhakikisha wadau wanaweza kuja na maazimio ya moja kwa moja ili kuwasaidia kuzalisha bidhaa ambazo ni bora ili kuweza kulinda walaji vilevile na kujiongezea masoko.

Mkurugenzi wa Udhibiti Ubora (TBS),Bw. Lazaro Msasalaga aliwashauri wadau hao kuzingatia kanuni za uzalishaji na uhifadhi bora na salama ili kuepuka kupoteza masoko na kero ya kukutwa na bidhaa hafifu ambayo itawalazimu kuteketeza kwa gharama zao. 

Pia aliwashauri kuwasiliana na ofisi ya TBS mara kwa mara pale wanapohitaji msaada wa kitaalamu katika mnyororo mzima wa uzalishaji, uhifadhi na ufungashaji sahihi.

 Kaimu Mkuu wa Kanda ya kati TBS , Bi Salome Emmanuel aliwasisitiza wajasiriamali ambao bado bidhaa zao za mafuta hazijapatiwa nembo ya bora, kuchangamkia fursa ya bure kwa kutuma maombi kupitia SIDO ili waingie katika huduma ya bure kwa wajasiriamali wadogo haswa ukizingatia bidhaa ya mafuta ipo katika kiwango cha lazima.

Mafunzo haya yalihusisha wadau walioweza kushiriki katika kumbi mbalimbali zilizoandandaliwa lakini vilevile utembelewaji wa moja kwa moja wa wadau hao katika maeneo yao ya uuzaji au uzalishaji kama vile maeneo ya Pandambili,soko kuu la Singida na Tarafa ya Pahi.

Baadhi ya wadau hao walipongeza juhudi zinazofanywa na TBS katika kuhakikisha wanawasaidia wadau wa sekta mbalimbali kuzingatia viwango ili kuweza kupata masoko ndani na nje ya nchi na kuwa na ushindani huru sokoni.

  Hata hivyo waliitaka TBS kuhakikisha huu mpango wa mafunzo sambamba na kaguzi za mara kwa mara masokoni ni endelevu kwa bidhaa zote na haswa maeneo ya vijijini, ili kumlinda mlaji dhidi ya bidhaa hafifu na zile zilizokwisha muda wa matumizi au zisizotakiwa kabisa sokoni. 

Mpaka sasa wadau takribani 358 kutoka Kongwa, Chamwino, Mpwapwa, Kibaigwa na Kondoa wamefikiwa na mafunzo haya, ambapo maeneo ya Bahi, Dodoma jiji, Manyoni na Itigi watafikiwa kuanzia tarehe 28.09.2020.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com