Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TCAA WAJIBU MADAI YA HELKOPTA YA CHADEMA KUZUILIWA NA KUNYIMWA KIBALI


Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)  kilitoa taarifa leo Asubuhi kwamba Ratiba ya Mikutano mitano ya kampeni za  Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano kupitia chama hicho  Mh. Tundu Lissu imevurugika baada ya helkopta aliyokuwa aitumie kwenda kwenye mikutano hiyo  kukosa kibali cha Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA.).


Baada ya kutolewa kwa taarifa hiyo, Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imelitolea ufafanuzi swala hilo na kusema kuwa helikopta ya kampuni ya State Aviation iliyokuwa itumiwe na mgombea wa urais wa CHADEMA imepewa kibali cha muda mrefu (block permit) na TCAA kwa shughuli za kampeni za uchaguzi kuanzia tarehe 4 Septemba hadi tarehe 31 Oktoba 2020 na vibali hivi hutolewa kwa watoa huduma ili kuepuka kuomba vibali mara kwa mara pindi wanapopata wateja wao.

Mnamo tarehe 9 Septemba 2020, kampuni ya State Aviation iliomba kibali cha msamaha (exemption) ili iweze kumtumia rubani mwenye umri zaidi ya miaka 65 ambao ni wa juu Kwa mujibu wa sheria za usafiri wa anga kupitia Kanuni ya 15 ya Kanuni za Utoaji wa Leseni za Wataalam wa Usafiri wa Anga ya mwaka 2017. Msamaha huo ulikua unaombwa kwa ajili ya kampuni hiya kutoa huduma kwa wateja wake (CHADEMA) kwa safari iliyopangwa kufanyika tarehe 10 Septemba 2020

Msamaha huo haukutolewa kwani ni kinyume cha sheria na ungehatarisha maisha ya wateja wao na umma kwa ujumla na taarifa hiyo ilitolewa siku hiyo hiyo ya tarehe 9 Septemba 2020.

Aidha kwa taarifa hii, Mamlaka inakanusha kwamba hakuna ofisa yoyote yule wa TCAA aliyetoa taarifa kwa msafara wa Mhe. Lissu juu ya kutofanyika kwa safari hiyo kwani taarifa za kufanyika au kutokufanyika kwa safari ni mahusiano kati ya mtoa huduma na wateja wake. Aidha hakukuwa na mpango wowote ule wa safari (flight plan) uliowasilishwa na mtoa huduma kwa TCAA kwa tarehe 10 Septemba 2020 kwa mujibu wa taratibu na sheria. Hivyo basi ifahamike wazi kuwa safari hiyo haikupangwa na haikuwemo kwenye orodha .

TCAA inatoa wito kwa kampuni za ndege na wadau wake kuzingatia sheria na taratibu za usafiri wa anga, zinapotoa huduma ikiwa ni pamoja na kufanya maandalizi ya safari zao mapema kuepuka usumbufu usio wa lazima.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com