Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CHADEMA Tundu Lissu leo Septemba 6, 2020. atazindua kampeni Kanda ya Kusini (Lindi, Mtwara na Ruvuma) katika Uwanja wa Sabasaba, mjini Mtwara.
Jana alikuwa Kanda ya Nyasa, katika viwanja vya Nzovwe, jijini Mbeya ambapo pamoja na mambo mengine aliahidi kujenga maeneo maalum kwa ajili ya shughuli za Machinga na Mamalishe ambayo yatakuwa wazi usiku na mchana.
Lissu alisema baadhi ya wananchi huwa wanachelewa kufika kwenye miji yao wanapokuwa wametoka safarini na hivyo kukosa huduma za kununua mahitaji kwenye masoko kutokana na masoko hayo kufungwa .
“Tutajenga masoko maalum kwa kushirikiana na sekta binafsi kwenye maeneo mbalimbali ili machinga wetu wafanye biashara hapo kwa uhuru na kila mmoja atakuwa na chumba chake,” aliahidi.
Vilevile, Lissu alisema serikali yao itajenga majengo maalumu kwenye maeneo ya stendi za mabasi kwa ajili wa wauzaji vyakula, maarufu mamalishe na babalishe, ili wafanyie biashara zao huko kwa uhuru.