Urusi imesema kauli ya waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo, kwamba afisa mkuu wa serikali ya Urusi alihusika katika kumpa sumu kiongozi wa upinzani Alexei Navalny, haikubaliki.
Awali, Pompeo alisema inawezekana afisa mwandamizi wa serikali ya Urusi aliamuru Navalny apewe sumu aina ya Novichok, na kuongeza kuwa dunia nzima inajua kilichotokea.
Msemaji wa rais wa Urusi Vladimir Putin amesema nchi yake inayo maslahi katika kujua undani wa yaliyomfika Navalny, na kuitaka Ujerumani kutoa ushirikiano kwa kuipa Urusi matokeo ya vipimo vya Navalny.
Mapema leo, Waziri Mkuu wa Italia, Giussepe Conte alinukuliwa akisema ameambiwa na Rais Putin kuwa uchunguzi utafanyika kubainisha ukweli kuhusu masaibu ya Alexei Navalny, lakini baadaye Urusi imekanusha hilo, ikisema yumkini Conte alielewa vibaya.
Navalny aliugua ghafla wakati akifanya kampeni kuelekea uchaguzi we serikali za mitaa utakaofanyika Ijumaa na Jumapili nchini Urusi.
-DW
Social Plugin