Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

VIJIJI 73 KATI YA 77 MISENYI VYAPATIWA UMEME

 
VIJIJI 77 kati ya vijiji 73 vya wilaya ya Missenyi mkoani Kagera vimepelekewa huduma ya umeme na vijiji 4 bado havina umeme.

Hayo yamesemwa jana (Jumanne, Septemba 29, 2020) na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa wakati akizungumza na wakazi wa kata ya Kassambya, katika mikutano uliofanyika kwenye uwanja wa Mashujaa, wilayani Missenyi, mkoani Kagera.

Amevitaja vijiji ambavyo havina umeme na vipo kwenye mpango wa kupelekewa umeme kuwa ni vijiji vya Buchurago, Katano, Kakunyu na Bugango.

Akizungmzia sekta ya mifugo ambayo imetajwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020 hadi 2025 kuanzia ukurasa 47-52, Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali ya Chama Cha Mapinduzi imeisimamia vizuri sekta ya mifugo ili kuhakikisha wafugaji wanapata manufaa.


“Shilingi milioni 23 zimetumika kukarabati machinjio ya Bunazi hapa Misenyi, pia tumerahisisha uuzaji wa mazao ya mifugo kwa kufuta tozo kero 114 katika sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi na kuimarisha masoko ya mazao ya mifugo kwa kuhamasisha uanzishwaji wa viwanda vya kuchakata mazao ya mifugo,” alisema.

Alisema Serikali imepanga kuanzisha vituo vya kisasa vya uchunguzi wa magonjwa ya mifugo katika mikoa 18 ambayo haina vituo, kuimarisha huduma za tiba za mifugo kwa kuhakikisha kila wilaya ina maabara, kliniki na daktari wa mifugo.

Mheshimiwa Majaliwa ambaye yuko mkoani Kagera kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli alitumia fursa hiyo kumnadi mgombea ubunge wa jimbo la Nkenge, Dkt. Florent Kyombo na wagombea udiwani 13 wa CCM wa kata za wilaya hiyo. Mgombea udiwani wa kata ya Kassambya, Bw. Yusuph Jumbe na wenzake sita, wamepita bila kupingwa.

Kuhusu barabara, Mheshimiwa Majaliwa alisema sh. bilioni 3.57 zilitolewa kupitia Wakala wa Barabara za Mjini na Vijijini (TARURA) kwa ajili ya ujenzi na matengenezo ya barabara za wilaya hiyo zikiwemo barabara za Bukwali-Kashenye-Bushango, Ngorogoro-Kyabugombe, Mabuye –Itara na Ruzinga - Mugongo.

Alizitaja barabara nyingine kuwa ni za Gera – Ishozi – Ishunju, Nyankele – Kilimilire, Mabale–Mwemage-Kyaka, Nyankele-Nyamilembe–Kenyana na Kituntu–Bwengabo. Alisema mwaka 2020/2021, sh. milioni 711.6 zimetolewa kupitia TARURA kwa ajili ya ujenzi na matengenezo ya barabara kwa muda maalum.

(mwisho)



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com